Kenya imekaribisha kundi la kwanza la watalii wa kigeni waliofika chini ya mfumo uliorahisishwa wa kuingia ambayo inatumai itawahimiza wageni zaidi.
Idara ya huduma za uhamiaji ya serikali ilisema Ijumaa "waliofika bila viza" walitua Nairobi kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa na wengine wanatarajiwa kuwasili siku zijazo.
Katibu Mkuu wa Uhamiaji na Huduma kwa Raia Julius Bitok alisema mahitaji ya viza yataondolewa kwa wasafiri wote kwenda Kenya bila kujali utaifa.
Chini ya mfumo mpya, wasafiri wanaomba mtandaoni ili kupata idhini ya usafiri wa kielektroniki (ETA) na kulipa ada ya $30.
"Hivi sasa... nchi zote duniani zikiwemo Afrika, Asia, Amerika, Australia, na kote duniani, zina uwezo wa kuja bila visa," alisema wakati wa uzinduzi wa mpango huo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi.
Nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda hazitahitajika kulipa ada ya $30, ili kupata idhini ya usafiri wa kielektroniki (ETA).
Hii ni kwa muda wa miezi sita.
Mwaka jana Rais William Ruto alitangaza kuwa Kenya itakuwa "nchi isiyo na viza" na mahitaji yaliyopo yangeondolewa Januari.
Hata hivyo, Jumanne iliyopita Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya ilionya mfumo mpya wa ETA ulikuwa "katika mchakato wa maendeleo na utekelezaji."
Kulingana na takwimu za wizara ya utalii, idadi ya watalii waliofika mwaka 2022 iliongezeka hadi milioni 1.54, lakini bado ilikuwa chini ya idadi iliyokuwa inapokelea kabla ya janga la Uviko 19.
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii ya Kenya Francis Gichaba alitoa matumaini mnamo Novemba kwamba idadi hiyo inaweza kuwa juu zaidi ya milioni mbili katika mwaka wa hivi karibuni wa kifedha, na kupita idadi ya 2019 ya milioni 1.9.