Upinzani umekuwa ukiitisha maandamano kupinga sheria ya fedha inayolaumiw akusababisha kupanda gharama ya maisha Picha:  Reuters 

Rais wa Kenya, William Ruto, ametangaza Ijumaa kuwa maandamano yaliyoitishwa wiki ijayo na viongozi wa upinzani hayataruhusiwa kufanyika kutokana na misururu ya maandamano yaliyosababisha watu 15 kufariki na mali ya zaidi ya dola milioni tano kuharibika.

Rais Ruto amedai kuwa upinzani una njama ya kuhujumu utawala wake na maandamano haya sio kwa maslahi ya Wakenya kama inavyodaiwa.

''Maandamano haya hayatafanyika. Nisikilize kwa makini: huwezi kutumia njia zisizo za kisheria, nje ya katiba kutafuta mamlaka nchini Kenya." Alisema Rais akihutubia waandishi wa habari katika uzinduzi wa barabara.

Muungano wa upinzani, Azimio, ulitangaza kuwa utaandaa maandamano mengine wiki ijayo kuanzia Jumatano hadi Ijumaa, na kila wiki baada ya hapo hadi malalamiko yao yasikilizwe.

Muungano huo umekuwa ukipinga sheria ya fedha iliyoidhinishwa na bunge licha ya kuwa wawakilishi wengi wa upinzani walikosa kuhudhuria kikao hicho cha kupigia kura.

Miongoni mwa masuala tata katika sheria hiyo ni ongezeko la ushuru katika sekta mbali mbali, pamoja na kuanzishwa kwa kodi mpya ya makazi, ambayo wengi wamelalamikia imesababisha gharama ya maisha kupanda kupita kiasi.

Hasara iliyotokea

Jumatano maelfu ya watu walishiriki maandamano katika miji mbali mbali nchini Kenya, yaliyoishia kwa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.

Polisi walitumia bomu ya machozi na katika baadhi ya maeneo wameshutumiwa kutumia risasi kuwatawanya waandamanaji.

Waziri wa Usalama wa ndani Kithure Kindiki alitangaza Alhamisi kuwa zaidi ya watu 300 wamekamatwa na polisi wakihusishwa na uharibifu uliotokea wakati wa maandamano.

Waziri wa barabara Kipchumba Murkomen naye alikisia hasara iliyotokea kufuatia maandamano hayo kuwa zaidi ya dola milioni tano.

Awali Jumatano kiongozi wa Upinzani Raila Odinga alitangaza kusitishwa kwa maandamano hayo baada ya ripoti za maafa, akisema kuwa amechukua uamuzi huo 'kulinda usalama wa Wakenya'.

Hata hivyo kufikia Ijumaa asubuhi alibatili msimamo wake na kuwaunga viongozi wengine wa Upinzani waliosisitiza kuendelea na maandamano wiki ijayo.

TRT Afrika
Reuters