Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC-AU) limetimiza miaka 20, toka kuanzishwa kwake.
Katika risala yake, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa bara la Afrika limeshindwa kunyamazisha silaha kwa wakati muafaka, huku mabadiliko ya uongozi yasiyofuata misingi ya kidemokrasia yakitamalaki.
"Mambo kama hayo yametufanya tuendelee kushuhudia migogoro isiyokwisha barani Afrika," amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo wa Tanzania amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utambuzi wa mapema wa migogoro barani Afrika na kuhusisha wanawake na vijana katika michakato ya utafutaji amani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amesema ni vyema kwa bara la Afrika kufanya tathmini ya uhuru wa bara hilo, hususani utekelezwaji wa mabadiliko ya uongozi yenye kuzingatia katiba.
"Tunapoadhimisha miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama, ni vyema tujiulize, ni nchi ngapi barani Afrika zinazoruhusu waangalizi wa uchaguzi kuhudhuria na kushuhudia michakato hiyo," alihoji Mahamat.
Mnamo mwezi machi 2022, Tanzania ilichaguliwa kuhudumu kwenye nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa miaka miwili hadi mwezi Machi 2024 ambapo muda wa kuhudumu ulifikia kikomo.
Jukumu la Baraza
Barala la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lenye wanachama 15 wa kuteuliwa, lina jukumu la kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza.
Hadi sasa, baraza hilo linasimamia shughuli 10 za kulinda amani katika nchi 17 barani Afrika, likijumuisha walinda amani zaidi ya 70,000.
"Operesheni hizi ni nyenzo muhimu katika zana muhimu za kudhibiti migogoro. Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, operesheni za amani zinazoongozwa na Waafrika zimefanya jitihada za kushugulikia vitisho vya machafuko barani Afrika," imesomeka sehemu ya chapisho katika tovuti ya African Center for Strategic Studies.
Busara za wazee
Kwa namna ya pekee, viongozi wa zamani wa Afrika walipata nafasi ya kuunda jopo la wazee kwenye sherehe hizo, wakitoa mang'amuzi yao ya safari ya bara la Afrika ndani ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.
Olusegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Nigeria amesema kuwa bara lilichukua uamuzi sahihi kuanzisha chombo hicho chenye jukumu la la kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza.
"Tulichukua njia sahihi kwani kuna baadhi ya mafaniko tumeyapata japo kuna baadhi ya maeneo hatukuweza kufanya vizuri," amesema Obasanjo.
Rais wa zamani wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa upande wake amesema migogoro mingi inayotokea barani Afrika inasababishwa na 'kukosekana kwa uongozi'.
Kulingana na Kikwete, ukabila, upendeleo na ukosefu wa taasisi imara umechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa migogoro ya aina hii.
"Ni kawaida sana kuona mshindwa anatangazwa mshindi wakati mshindi anakuwa mshindwa kwenye michakato mingi barani Afrika," ameongeza.
Nchi 15 tu kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika ndio wajumbe wa Baraza hilo na wajumbe wa sasa ni; Tanzania, Uganda , Djibout, Cameroon, DRC, Equatorial Guinea ,Afrika Kusini, Angola, Botswana, Cote d’Ivoire , Gambia, Nigeria, Sierra Leone, Misri na Morocco.
Maadhimisho hayo, yametoa fursa kwa Waafrika wote wenye kuitakia mema Afrika kutoa maoni yao ya kuliimarisha Baraza ili liweze kushughulikia changamoto za kiusalama barani Afrika ambapo wageni takriban 120 kutoka nchi mbalimbali wamehudhuria maadhimisho hayo.