Mwaka huu, Siku ya Afya ya Akili Duniani inalenga katika kuweka kipaumbele cha afya ya akili sehemu za kazi/ Picha Wengine.

Huku dunia ikiadhimisha siku ya afya ya akili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema ni lazima afya ya akili ipewe kipaumbele.

"Ulimwenguni kote, takriban mtu mmoja kati ya kila watu nane wanaishi na ugonjwa wa akili. Hakuna jamii iliyoachwa. Kujiua bado ni sababu kuu ya vifo kati ya vijana, na mamilioni ya watu wanaendelea kuteseka kimya kimya," Gutteres amesema katika taarifa yake.

Mwaka huu, Siku ya Afya ya Akili Duniani inalenga katika kuweka kipaumbele cha afya ya akili maeneo ya kazi.

"Afya mbaya ya akili inaweza kusababisha kupungua kwa utendaji na kutokuwepo kazini. Huzuni na wasiwasi pekee husababisha hasara ya takriban bilioni 12 kazini kila mwaka," limesema Shirika la Afya Duniani WHO.

Asilimia 60 ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka kumi na tano wako kwenye ajira, wakitumia muda wao mwingi katika sehemu za kazi.

"Maeneo salama ya kazi yenye afya yanaweza kutoa hali ya kusudi, muunganisho na uthibiti, ilhali mazingira ya kazi ya ukandamizaji au machafuko yanaweza kuathiri sana afya ya akili ya wale wanaofanya kazi huko," Gutteres ameongezea.

WHO inaonya kuwa ajira za malipo ya chini au zisizo salama mara nyingi huwaacha wafanyakazi katika hatari za kisaikolojia.

"Kazi ni muhimu kwa ustawi; lakini ustawi pia ni muhimu kwa kazi. Waajiri wanaposhughulikia hatari kwa afya ya akili kwa wafanyakazi wao, huongeza ari, kupunguza utoro, na kuongeza ushiriki wa wafanyakazi na tija, kuimarisha biashara zao na uchumi wetu," Gutteres ameongezea.

TRT Afrika