Aprili 2022, kasuku 122 walikamatwa kutoka kwa wafanyabiashara karibu na Bunagana, iliyoko kwenye mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ndege hao ni kasuku wa Kiafrika wa kijivu.
Watatu walikufa na 119 waliobaki walipelekwa katika kituo cha elimu ya uhifadhi wanyamapori cha Uganda, yaani Uganda Wildlife Conservation Education Centre, UWEC.
Sasa Kasuku 55 kati ya 119 wamerejeshwa porini katika Hifadhi ya Kitaifa ya Kibale Magharibi mwa Uganda.
" Hii ni hatua ya kupambana na biashara haramu na usafirishaji haramu wa viumbe hawa walio katika hatari," amesema David Musingo,meneja wa UWEC,
" Imechukua zaidi ya mwaka kuwaachilia kasuku hao kwasababu walikuwa vielelezo katika kesi za mahakama," ameongezea Musingo,meneja wa UWEC " mahakama imetupa kibali cha kuwaachilia."
Kasuku wa Kiafrika wa kijivu ameorodheshwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Uhifadhi na Mazingira kama ndege anayesakwa kwa ajili ya biashara zaidi ulimwenguni.
Takwimu za idadi ya ndege hao nchini Uganda bado ni chache.
" Kasuku wa Kiafrika wa kijivu ni kati ya ndege zinazouzwa zaidi kihalali. Kutekwa kwao porini kunatesa, kunaumiza, na kuchukiza aina hiyo ya ndege ”amesema Edith Kabesiime, meneja wa kampeni ya wanyamapori katika shirika la World Animal Protection.
Ulimwenguni inakadiriwa kuwa kuna kati ya kasuku wa kijivu kati ya elfu arobaini na milioni moja.