Kanisa pia limesema litarudisha mchango wa zadii ya dola 1500 (Shilingi  200,000) zilizotolewa na Gavana wa Nairobi kwa kanisa hilo Novemba 17, 2024/ Picha Rais William Ruto.

Kanisa la Katoliki nchini Kenya limekataa mchango wa Rais William Ruto alioutoa katika kanisa la Soweto jijini Nairobi Novemba 17, 2024 pindi alipohudhuria misa katika kanisa hilo mwishoni mwa juma.

Rais William Ruto alitoa mchango wa zaidi ya dola 15, 444 ambazo ni sawa na shilingi milioni 2 kwa ajili ya wa ujenzi wa nyumba ya kasisi wa kanisa, na kuongeza mchango wa dola 4, 600 ambazo ni sawa na shilingi 600,000 kwa ajili ya kwaya ya kanisa.

Wakati huo huo pia, ameahidi mchango mwengine wa zaidi ya dola 23,000 ( milioni 3) kwa ujenzi huo.

Rais pia aliahidi kutoa mchango wa basi la kusafiria kwa ajili ya kanisa.

Kanisa pia limesema litarudisha mchango wa zadii ya dola 1500 ( shilingi laki mbili) zilizotolewa na Gavana wa Nairobi kwa kanisa hilo.

Barua kutoka kwa Askofu Mkuu Philip Anyolo imesema kuwa mchango huo unakiuka muswada ambao ulipendekezwa na Rais Ruto kuhusu michango ya harambee.

Rais Ruto alipendekeza Julai 2024 kuwepo na sheria ya kuongoza michango au harambee.

Amesema hiyo itazuia maafisa wa serikali na umma kushiriki katika harambee, ambayo ina nia ya ufisadi kutoka kwa wanasiasa na kuwahonga wananchi.

Kanisa limekataa mchango huu siku chache baada ya Muungano wa Maaskofu kuandika barua ambayo iliishutumu serikali ya Rais William Ruto kwa kushindwa kutatua baadhi ya changamoto za wananchi.

Katika barua hiyo ya Novemba 14, 2024 kanisa lililalamikia sera mpya za afya na elimu ambazo zimewekwa na uongozi wa Rais Ruto.

Pia lililalamika kuzorota kwa hali ya usalama nchini hivyo kusababisha vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji, utekaji nyara na watu kupotea bila maelezo yoyote.

Rais Ruto alijibu madai hayo ya Kanisa kwa kusema kuwa ni muhimu ukosoaji ufanywe kwa kuzingatia ukweli.

Ni baada ya kashfa hizo za kanisa dhidi ya serikali yake, ndipo Rais Ruto alipohudhuria misa ya Jumapili katika kanisa la Katoliki la Soweto jijini Nairobi Novemba 17 na hapo ndipo alipotoa mchango wake.

Uamuzi huo wa kanisa wa kukataa mchango wa serikali pia umepata shinikizo kutokana na kampeni ya wananchi baada ya kumuandikia barua Askofu Mkuu na pia kupitia mitandao ya kijamii, kulitaka kanisa kurudisha mchango huo na kutaka kusimamia msimamo wake wa kuiwajibisha serikali.

TRT Afrika