Wawindaji huua wanyama kwa ajili ya sehemu zao ambazo huwauzia waganga wa kienyeji. Picha: Reuters

Na Ferdinand Mbonihankuye

Utumiaji wa sehemu za wanyama pori na mimea katika dawa za kienyeji ni jambo la kawaida nchini Burundi lakini athari kwa wanyamapori sasa inazua mtafaruku.

Burundi ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya matumizi ya dawa za asili duniani. Kulingana na Shirika la Afya Duniani, WHO, karibu 80% ya watu barani Afrika wanategemea aina za dawa za kienyeji ili kukidhi mahitaji yao ya afya.

''Katika nchi ambazo data za kina zaidi zinapatikana, asilimia ya watu wanaotumia dawa za asili ni kati ya 90% nchini Burundi na Ethiopia, hadi 80% nchini Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Afrika Kusini; 70% nchini Benin, Cote d'Ivoire, Ghana, Mali na Rwanda na 60% nchini Tanzania na Uganda,'' WHO inasema.

Lakini kuna wasi wasi nchini Burundi ambapo baadhi ya watu hukimbilia uwindaji haramu wa wanyama pori pamoja na ukataji miti kwa ajili ya kutafuta dawa za kienyeji.

Wawindaji huwaua wanyama ili kupata ngozi na viungo vyao, ambavyo waganga wa tiba asili hununua hasa katika mikoa iliyo karibu na misitu na mbuga za wanyama.

Wanyama Kupungua Sehemu za wanyama huuzwa hadharani katika masoko ya ndani kwa ajili ya dawa za asili zinazothaminiwa sana nchini.

Mamlaka mara nyingi husema baadhi ya wawindaji hao huchoma misitu na kuharibu makazi asilia ya wanyama hao na kwamba wanaua wanyama pori wakiwemo simba marara, puma, chatu, twiga, fisi na swara kwa ajili ya matibabu.

Hili linatishia wanyamapori nchini.

Madaktari wa tiba asilia nchini Burundi wanaamini kuwa viungo vya wanyama hao wanavyovitumia katika utayarishaji wa dawa za kienyeji vina nguvu katika kuponya magonjwa mbalimbali hatari na pia vinafanya kazi dhidi ya sumu.

Lakini hata wale wanaohusika wanakubali kwamba idadi ya wanyama na aina ya mimea inayotumiwa kwa dawa za jadi inapungua.

''Baadhi ya mitishamba hii na wanyama fulani wametoweka kutoka kwenye misitu ya Burundi,'' Ntakanan Irimana, daktari wa tiba asili aliiambia TRT Afrika.

Ntakanan Irimana kutoka wilaya ya Muruta katika mkoa wa Kayanza anasema wakati mwingine wanasafiri kwenye misitu katika maeneo ya mpakani kabla ya kupata baadhi ya aina za mimea na wanyama.

Mila dhidi ya idhini ya Uwindaji

''Aina kadhaa za wanyama kwa sasa ni adimu, na ndege fulani hawapatikani popote nchini Burundi, hasa tai na ibis,'' Mganga mwingine wa tiba asili aliiambia TRT Afrika.

Nchini Burundi, uwindaji unachukuliwa kuwa mila na wengi wao hawaoni kuwa ni hatari hata katika muktadha wa kupungua kwa idadi ya wanyama pori. Hii pia inaungwa mkono na umaarufu wa dawa za asili nchini.

"Tunaua mnyama ambaye ngozi yake ni dawa. Tunang'oa kile ambacho kina manufaa kwetu", anasema mganga wa kienyeji katika jimbo la Kayanza ambaye hakutaka kutajwa jina.

Ingawa kuna sheria zinazosimamia wanyamapori, uwindaji na ulinzi nchini Burundi, ni nadra kuzingatiwa.

Abel Nteziryayo, ambaye ana jukumu la kulinda hifadhi ya asili ya Kibira, alisema ''waganga wote wa jadi wanahitaji idhini'' kabla ya kuingia katika hifadhi za asili za Burundi.

Alilalama kuwa wawindaji haramu huingia mara kwa mara katika misitu hii mikubwa na hifadhi za wanyama wakati mwingine bila kugunduliwa na walinzi wa hifadhi ambao hawatoshi kuchunga misitu yote.

Hali hii huwaacha wanyama pori na miti katika hali ya hatari .

Baadhi ya wawindaji huchoma sehemu za misitu kwa ajili ya kujaribu kuwaua wanyama hao, ambao wakati mwingine hukimbilia katika jamii zilizoko karibu na misitu hiyo ambako nako si salama.

Mamlaka kuwa makini

Wataalamu wanasema wanyama hao wanahitaji maeneo yaliyohifadhiwa ili waweze kuzaliana na mimea iliyo hatarini inahitaji kutunzwa na kulindwa huku upandaji miti ikiwa mojawapo ya hatua muhimu zinazoweza kuchukuliwa

Mamlaka zimeongeza kampeni za uhamasishaji ili kusitisha tabia hiyo. Pia wamekuwa wakichukua hatua za adhabu kali dhidi ya wawindaji wanaotiwa mbaroni.

Kwa mfano, Septemba mwaka jana, watu wasiopungua sita walikamatwa kwa tuhuma za kuua sokwe kinyume cha sheria katika kijiji cha Mpfunda karibu na Hifadhi ya Mazingira ya Kibira mkoani Kayanza.

Washukiwa hao walinaswa wakigawana nyama ya mnyama waliyedaiwa kumuua. Mkuu wa huduma za ulinzi wa Hifadhi ya Mazingira ya Kibira, Abel Nteziryayo aliiambia TRT Afrika kuwa watu hao wamevunja sheria za utunzaji wa mazingira kwa sababu sokwe ni sehemu ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka.

“Kama waganga wa kienyeji wanahitaji ngozi za aina fulani za wanyama, inabidi waombe kibali kutoka kwa wizara inayosimamia mazingira”, anasema.

Wakati mamlaka zinafanya juhudi za kutekeleza kanuni za mazingira, wataalam wanasema kuna haja ya kutafuta njia zaidi za kuongeza idadi ya wanyama pori na kurejesha misitu iliyopotea.

Hata hivyo, pia wanaeleza kuwa bila njia mbadala za dawa za kienyeji au vyanzo vyake, hali inaweza kubaki kuwa ngumu.

TRT Afrika