Na Ramadhan Kibuga
TRT Afrika. Bujumbura, Burundi
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amefanya mabadiliko madogo ya Baraza lake la Mawaziri. Mawaziri wanne wapya wameteuliwa kushikilia wizara za Afya,Kilimo na Ufugaji Afrika ya Mashariki pamoja na Utumishi wa Umma.
Waziri mpya wa Afya ni Dkt. Lidouine Baradhana ambaye anachukua nafasi ya Dkt. Sylvie Nzeyimana.
Gervais Abayeho ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa wa Afrika ya Mashariki ,Vijana , Michezo na Utamaduni . Bwana Abayeho alikuwa hadi sasa ni Balozi wa Burundi nchini Tanzania. Anachukua nafasi ya Ezechiel Nibigira.
Aidha Rais wa Burundi ameteuwa Waziri mpya wa Kilimo, Ufugaji na Mazingira Prosper Dodiko na kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Dk Sanctus Niragira. Prosper Dodiko alikuwa Katibu wa kudumu kwenye wizara hiyo.
Naye Venuste Muyabaga ni waziri mpya wa Utumishi wa Umma na Ajira akichukua nafasi ya Deo Rusengwamihigo.
Mabadiliko haya ya Baraza la Mawaziri yanakuja baada ya malalamiko mengi kusikika nchini kwamba baadhi ya mawaziri wameshindwa kuwajibika.
''Rais amefanya vizuri, Wizara ya Afya na Wizara ya Kilimo naweza kusema ilikuwa ni maiti hai. Maeneo hayo kumejaa hakika kilio cha raia. Lakini mageuzi makubwa yanahitajika zaidi mpaka tuone maisha yetu yanabadilika.'' Alisema Claire Niyonzima kutoka kata ya Bwiza katikati mwa jiji la Bujumbura
Changamoto na kashfa za wizara
Waziri mpya wa Afya Dk Lidouine Baradahana anarithi wizara ya afya yenye changamoto nyingi na ambayo imelalamikiwa kupita kiasi.
Mwishoni mwa Septemba bunge lilisikiliza malalamiko ya wizara hiyo ikiwa ni pamoja na hali ya kutisha ya idadi kubwa ya Madaktari wanaozidi kuondoka katika hospitali za Umma na kwenda kuhudumu ugenini na hasa katika nchi jirani.
Lakini pia uhaba wa vifaa vya kazi hospitalini na kutatiza utekelezwaji wa hatua za serikali za kujifungua bure kwa kinamama wajawazito pamoja na matibabu ya bure kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.
Nayo Wizara ya Kilimo na Ufugaji ambayo pia imepata msimamizi mpya imekuwa inalalamikiwa sana na wakulima baada ya raia kujikuta wanakosa mbolea na mbegu ilihali msimu wa kilimo cha masika tayari umeanza.
Changamoto hii inatazamiwa kuwa na athari kubwa nchini Burundi kwani asilimia 80 ya raia wake ni wakulima. Inahofiwa kwamba hali hiyo ya ukosefu wa mbolea inaweza kukwamisha uzalishaji na mavuno.
Kwa upande mwingine ,Wizara ya Utumishi wa Umma ambayo nayo pia imehusishwa na mageuzi ilijikuta siku za nyuma katika kashfa ya kuwaajiri mlango wa nyuma waalimu pamoja na kughushi mitihani.
Marie Inarukundo kutoka kata ya Musaga anasema ndoto yake kubwa ni kuona mageuzi upande wa sheria, ''Mimi kama sijaona mabadiliko kwenye wizara ya sheria kwangu hamna chochote. Hii nchi imeharibiwa na kukosekana utendaji haki sawa kwa wote. Rushwa imetawala pale. Ningempongeza saana Rais kama angegusa huko pia. Lakini nina imani hata wale ambao hawakuguswa.....watajirekebisha,'' alisema Marie.
Mabadiliko hayo yamezihusu wizara nne pekee kwa jumla ya wizara 15 zinazounda Serikali ya Burundi.