Msumbiji inakabiliwa na machafuko yanayoongezeka yanahusishwa na uchaguzi wa Oktoba wenye mgogoro. / Picha: AFP

Kutokana na machafuko ya kisiasa nchini Msumbiji, Shirika la ndege la Turkish Airlines limesitisha safari za kuelekea mji mkuu Maputo zilizokuwa zimepangwa kufanyika Alhamisi.

Safari za ndege kati ya Johannesburg-Maputo na Istanbul-Maputo zimesitishwa, shirika hilo la ndege lilisema katika taarifa.

Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na hali ya sintofahamu inayoendelea katika eneo hilo kufuatia mahakama ya juu zaidi nchini humo kuthibitisha siku ya Jumatatu, ushindi wa chama tawala cha Frelimo ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1975.

Mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo, alitangazwa mshindi kwa takriban asilimia 65 ya kura, matokeo ambayo yalipingwa na makundi ya upinzani yanayodai kuwa kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi uliofanywa Oktoba.

Ongezeko kubwa la uhalifu

Machafuko hayo pia yamesababisha ukiukwaji mkubwa wa usalama, ikiwa ni pamoja na kutoroka kwa watu wengi katika gereza karibu na Maputo ambapo zaidi ya wafungwa 6000 walikimbia wakati wa ghasia siku ya Jumatano.

Mapigano hayo ndani ya gereza hilo yalisababisha vifo vya watu 33 na wengine 15 kujeruhiwa. Vifo vya hivi punde vilileta idadi ya vifo nchini kufikia 151 tangu Oktoba 21, kulingana na Plataforma Decide, shirika la kufuatilia uchaguzi.

Ongezeko kubwa la uhalifu linatarajiwa katika mji mkuu wa Maputo katika muda wa saa 48 zijazo, alisema Kamanda Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo, Bernardino Rafael.

TRT World