Waziri wa Mambo ya Nje Ali Youssef akizungumza wakati wa mahojiano maalum huko Port Sudan. / Picha: AA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Youssef ameipongeza Uturuki kwa uungaji mkono wake mkubwa kwa Sudan huku kukiwa na mzozo unaoendelea Afrika Kaskazini.

Tangu Aprili 2023, Sudan imekuwa ikikabiliwa na mapigano makali kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuhusu mageuzi ya kijeshi na masuala ya ushirikiano.

Mzozo huo umegharimu maisha ya zaidi ya 20,000, mamilioni ya watu kuyahama makazi yao, na kuwaacha zaidi ya milioni 25 wakihitaji msaada wa kibinadamu, kulingana na UN.

Siku ya Alhamisi, Youssef alitathmini uhusiano "wa kuaminika na wa kihistoria" kati ya Sudan na Uturuki, akisema kuwa uhusiano huu umeimarisha mawasiliano kati ya wananchi wa kutoka nchi hizo mbili kwa karne nyingi.

Amesisitiza kuwa Uturuki imeelezea kuunga mkono mamlaka ya Sudan katika majukwaa yote na kusema: "Chini ya uongozi wa Rais (Recep Tayyip) Erdogan, Uturuki imeonyesha msimamo wa ukarimu na chanya kwa watu na taifa la Sudan wakati wa vita."

Youssef pia ameonyesha matumaini kuhusu pendekezo la Erdogan la upatanishi kati ya Sudan na UAE kutatua mizozo inayoendelea.

"Tunatumai kwamba mipango iliyowekwa, ikiwa ni pamoja na pendekezo la kiongozi mwenye busara na uzoefu Erdogan, ambaye alionyesha utayari wake wa kupatanisha Sudan na UAE baada ya upatanishi uliofanikiwa kati ya Ethiopia na Somalia, itafanikiwa," alisema.

Waziri wa Sudan alisema kuwa RSF ilikataa kufuata masharti ya "Azimio la Jeddah" lililotiwa saini Mei 2023.

"Vita vya Heshima" Youssef amesisitiza kuwa vita vya Sudan vimewasababishia watu wa Sudan mateso makubwa, akielezea mzozo huo kama "Vita vya Heshima" kutokana na mateso wanayovumilia watu.

"Wananchi wa Sudan wanakabiliwa na ukiukwaji mkubwa katika historia yake. Hakuna mtu duniani ambaye amefanyiwa yale ambayo watu wa Sudan wamevumilia. Kwetu sisi vita hivi vinaitwa ''Vita vya Heshima'' kwa sababu ni heshima ya watu wa Sudan. ambao wamejeruhiwa," Youssef alisema, akisisitiza kwamba "ukaidi wa watu" ulikuwa na jukumu muhimu katika ushindi wa hivi karibuni wa jeshi la Sudan.

Youssef pia alitoa wito wa kutafutwa suluhi la amani katika mzozo huo, akielezea masharti mawili muhimu: kubanduliwa kwa vikosi vya majeshi yote na kuanzishwa kwa jeshi la umoja wa Sudan, na kutengwa kwa viongozi wa RSF katika nafasi yoyote ya kisiasa katika kipindi cha baada ya vita.

Amesisitiza kuwa suluhu la kuleta amani lazima liamuliwe na uchaguzi huru na wa haki, ambapo watu wa Sudan wataamua uongozi wao. Mwanasiasa huyo, akiashiria ripoti ya Kamati ya Wataalamu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, alisema kuwa UAE ilitoa msaada wa kijeshi kwa RSF nchini Sudan kupitia uwanja wa ndege nchini Chad.

Alisema hilo limethibitishwa na taasisi mbalimbali za Marekani na Magharibi.

'Hakuna baa la njaa Sudan'

Kuhusu uhusiano wa kigeni wa Sudan, alisema uhusiano wa Sudan na Urusi pia uko "wazi na uko katika kiwango kizuri," akiongeza kuwa Urusi ilipinga rasimu ya azimio la Uingereza dhidi ya Sudan katika Umoja wa Mataifa.

Alisema kuwa msimamo wa Urusi ulitoa ujumbe muhimu kwa madola ya Magharibi, kupinga uwezo wao wa kulazimisha matakwa yao kwa Sudan na mataifa mengine.

Akisema kwamba nchi za Marekani na Umoja wa Ulaya zinaona vita vya Sudan kama vita tu kati ya pande mbili au vita kati ya majenerali wawili, ameongeza: "Hii ina maana kwamba wanashindwa kuona kinachotokea kama vita dhidi ya uhalali wa serikali ya sasa Sudan.

Huu ni ulaghai na upendeleo. Zaidi ya hayo, nchi hizi zinazungumzia haki za binadamu na njaa nchini Sudan.

Kinachotokea Sudan ni umaskini. Tunaweza pia kuona watu maskini nchini Marekani wamelala mitaani. Walakini, hakuna baa la njaa nchini Sudan kama nchi hizi zinajaribu kuonyesha."

TRT World