Wizara ya Ulinzi ya Gabon imesema maafisa nane wanaoshukiwa kumtesa hadi kumuua mwanajeshi anayedaiwa kuiba wamezuiliwa katika kesi ambayo imeitikisa nchi hiyo inayoongozwa na jeshi.
Majenerali wawili pia watahojiwa baada ya mkutano wa dharura ulioongozwa na kiongozi wa mapinduzi Brice Oligui Nguema, kulingana na taarifa ya Wizara iliyosomwa kupitia runinga ya serikali mwishoni mwa Jumatano.
Picha za mwili wa mwanajeshi huyo, Johan Bounda, uliokatwakatwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti zilizua vilio katika taifa hilo la Afrika ya Kati.
Mamlaka ziligoma kujibu kwa ahadi za uchunguzi, na Oligui mwenyewe alitembelea familia ya muathirika Jumatano, Siku ya Krismasi.
Waendesha mashtaka wanasema Bounda alishtakiwa kwa kujaribu kuiba katika nyumba ya mmoja wa wakuu wa jeshi, huku vyombo vya habari vikisema alipelekwa katika makao makuu ya idara ya usalama ya kijeshi, inayojulikana kama B2, kwa kuteswa.
Jeshi mapema mwezi huu liliondoa amri ya kutotoka nje usiku tangu lilipochukua mamlaka mnamo Agosti 2023.
Siku chache kabla, polisi walikuwa wamekamata makumi ya waandamanaji vijana huko Libreville kwa kukiuka amri ya kutotoka nje, huku wengine wakidai kuwa walinyolewa vichwa na viongozi kama adhabu.
Oligui ameahidi kuirejesha Gabon kwenye utawala wa kiraia, na wiki hii katiba mpya ilitolewa baada ya kuidhinishwa na wapiga kura wa Gabon mwezi Novemba.
Hakuna tarehe ya uchaguzi iliyowekwa.