Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amemteua Hajat Sharifah Buzeki kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Jiji la Kampala, huku Benon Kigenyi akiteuliwa kuwa Naibu wake.
Frank Rusa, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria amekuwa akikaimu nafasi hiyo.
Jukumu la mkurugenzi mkuu wa jiji ni kutoa mwongozo wa kimkakati na kufuatilia usimamizi bora wa mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Jiji la Kampala.
Jiji la Kampala lenye idadi ya watu zaidi ya milioni 4 limekuwa likimulikwa baada ya tukio lililosababisha watu zaidi ya 30 kufariki dunia kufuatia kuporomoka kwa jaa la taka la Kiteezi, mwezi Agosti.
Wakazi wengi wanatarajia kuwa uteuzi huu utakuwa chachu katika kuimarisha utoaji huduma na ukarabati wa miundombinu wa jiji hilo.
Majina ya Buzeki na Kigenyi yamewasilishwa kwa Tume ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya taratibu za kisheria na baada ya hapo watateuliwa rasmi na Mkuu wa Utumishi wa Umma.
Amekuwa Kamishna wa Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Idara ya Ukaguzi ya Wizara ya Utumishi wa Umma.