Mwanamke wa Sudan aliyekimbia makazi yake apumzika na mtoto wake katika kambi ya Zamzam, Kaskazini mwa Darfur, Sudan, Agosti 1, 2024. (Reuters/Mohamed Jamal Jebrel).

Na Tufail Hussein

Mapema mwaka huu, nilitembelea Sudan ili kujionea ukubwa wa mgogoro wa kibinadamu. Nilichokiona kilinishtua.

Familia nzima ilikuwa ikilazimishwa kuishi kwa mlo mmoja tu kwa siku kati ya wote, kambi za wakimbizi wa ndani zimezidiwa na idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao, na watu wamesimulia hadithi za kutisha za vurugu na ukatili. Lakini kitu kilichonishtua ni kutojali kwa jumuiya ya kimataifa.

Vita nchini Sudan vimesababisha njaa mbaya zaidi duniani na migogoro ya wakimbizi wa ndani. Zaidi ya watu milioni 11 ni wakimbizi wa ndani, imezidi wakazi wote wa London na Birmingham.

Nusu ya idadi ya watu nchini humo, inayofika watu milioni 25.6, wana uhaba wa chakula, ikimaanisha kuwa hawajui mlo wao ujao utakuja lini, na njaa sasa imefika katika eneo la Darfur huku vita hivyo vikiwafanya wakulima kuondoka kwenye ardhi yao, wakiacha masoko kuporwa, kusababisha njaa, na uksosaji wa misaada ya kibinadamu.

Pamoja na hayo yote jumuiya ya kimataifa tangu mzozo huo kuzuka mwezi Aprili 2023 imesalia kuwa kimya. Nilipokuwa nikitembelea kambi za wakimbizi wa ndani huko Port Sudan na Gedaref, sikuona timu hata mwana habari mmoja.

Bila shaka, kuna changamoto kubwa kwa waandishi wa habari kutokana na machafuko nchini kote, na waandishi wa habari wa Sudan wamekabiliwa na hatari kubwa kujaribu kuripoti mgogoro huo. Na licha ya vizuizi hivi, kumekuwa na ripoti nzuri katika miezi ya hivi karibuni.

Lakini bado ni muhimu sana kwa wingi wa habari kuendana na ukubwa wa tukio. Bila ya kuwa na ripoti ya vyombo vya habari, hatua ya kisiasa, kidiplomasia na ya kibinadamu, utulivu ambao Sudan inahitaji, hautapatikana.

Lakini kwa nini suala la Sudan limeshindwa kushughulikiwa? Kuna mambo kadhaa yanayochangia haya.

Dunia imebadilika

Kwa bahati mbaya, naamini kama ulimwengu umebadilika. Kudorora kwa uchumi wa dunia kwa miaka ya hivi karibuni kumezidisha shida duniani kote, ikiwa ni pamoja na umaskini na mateso ndani ya nchi yetu, Uingereza.

Katika jumuiya ya Islamic Relief UK, programu zetu za ndani zimeongezeka kila mwaka tunapojaribu kupunguza viwango vya umaskini vinavyoongezeka.

Cha kusikitisha ni kwamba, hii ina maana kwamba mateso ya watu katika nchi nyingine yamechukuliwa kuwa yasiyostahili kushughulikiwa.

Mtoto mwenye utapiamlo, mwenye umri wa miezi 17 akiwa katika wodi ya watoto ya Mother of Mercy huko Gidel, karibu na Kauda, ​​Juni 25, 2024, (Reuters/Thomas Mukoya).

Zaidi ya hayo, tumeona jinsi baadhi ya vyombo vya habari vinavyowakosoa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi Uingereza. Nani angefikiria miaka 30 iliyopita kwamba tungewapa kisogo watu wanaokimbia ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu?

Kwa bahati mbaya, ninaamini hii inaanza kuwa jinsi watu wengi wanavyowaona wale wanaoteseka, kama watu "wengine" ambao siku moja wanaweza kutishia maisha yao wenyewe, kwa sababu watu wengi hapa wanapambana na hali mbaya ya kiuchumi.

Katika miaka kumi hivi iliyopita, mizozo barani Afrika imeshindwa kushughulikiwa. Ni watu wangapi wanajua kuwa Somalia imekabiliana na ukame mbaya?

Au kwamba mgogoro wa kikatili umeharibu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo? Bara la Afrika mara nyingi linakashifiwa siku hizi, kwani imani potofu mbaya zimeenea kwamba migogoro ya kibinadamu ni kawaida tu huko.

Imani hizi zisizo na msingi, pengine zimechochewa na ubaguzi wa rangi na upendeleo wa kusudi au wa kutokusudia, zimefanya masuala ya Afrika kuwa rahisi kwa watu wa Magharibi kupuuza.

Kwa kweli, tumeona kwamba ni watu wa Sudan wenyewe ambao wanafanya zaidi kutunza familia zingine zilizoathiriwa na shida hii.

Jamii za ndani zimekaribisha wakimbizi wa ndani majumbani mwao na kushiriki chakula chao. Jamii hizo na makundi ya vijana wanajitahidi lakini bado juhudi hizo hazitoshi kutokana na ukubwa wa shida.

Suluhu za kisiasa

Kuna mamlaka za kimataifa nje ya bara zinazochochea migogoro kama vile mgogoro wa Sudan, na kupuuza vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.

Kukosekana kwa umakini kwa suala hili kumesababisha uharibifu mkubwa, kwa sababu kutojali kwa watu, kuna sababisha kutokuwa na shinikizo la kutosha kwa hatua za kisiasa. Muhimu zaidi, misaada ya kibinadamu haitatosha kamwe - suluhu za kisiasa na kidiplomasia zinapaswa kupatikana.

Mtazamo wa umma na ukosefu wa ufahamu haujasaidia mgogoro huo. Kulingana na kura ya maoni ya hivi majuzi ya Islamic Relief UK na shirika la upigaji kura la Savanta, asilimia 70 ya watu wazima wa Uingereza walisema hawajui lolote kuhusu mgogoro unaoendelea Sudan.

Aidha, muda wa mzozo wa Sudan unaendelea, vile vile mgogoro wa kutisha Gaza huko Palestina na hivyo kusababisha suala la Sudan kutopwa kipao mbele. Gaza imetawala vichwa vya habari vya kigeni tangu Oktoba 2023.

Tunachokiona katika eneo hilo ni ya kuhuzunisha, kwani jeshi la Israeli limefanya ukatili baada ya ukatili dhidi ya watu wa Palestina. Hii haimanishi kwamba Gaza inapaswa kutoriptiwa vizuri.

Watu huko Gaza wanakabiliwa na mzozo ambao haujawahi kutokea, na usitishaji wa mapigano bado hauonekani popote. Mashirika ya habari hayapaswi kuacha kuripoti juu ya uharibifu huo kabla ya kuisha kwa mateso ya Wapalestina.

Ajenda ya habari ya kimataifa mara nyingi inatatizika kuangazia hadithi nyingi za kibinadamu kwa wakati mmoja. Ukitazama nyuma miaka ya 2000, mgogoro katika jimbo la Darfur nchini Sudan ulikuwa habari kubwa, huku matukio nchini DRC yakipuuzwa.

Watu wa Sudan, waliokimbia vita vya Murnei katika jimbo la Darfur nchini Sudan, wanavuka mpaka kati ya Sudan na Chad huko Adre, Chad Agosti 4, 2023 (Reuters/Zohra Bensemra).

Katika miaka ya 2010, hadithi juu ya migogoro nchini Syria na Lebanon ziliingia kwenye magazeti mara kwa mara, lakini mgogoro wa Yemen ulisahaulika. Huku mizozo ikitokea Gaza, Ukraine na Lebanon mwaka huu, Sudan imeshindwa kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari.

Mwaka ujao, serikali na mashirika ya habari duniani kote yanahitaji kuwa makini na matukio ya Sudan na kufikiria upya jinsi yanavyoweza kusimulia hadithi za watu wa Sudan inavyostahili.

Jukumu la uandishi wa habari wa kimataifa ni muhimu sana, na linapaswa kuungwa mkono, kwani kuripoti bora kunaweza kumaanisha tofauti kati ya iwapo serikali zitahamasishwa kupata suluhu za kidiplomasia na za kibinadamu kwa migogoro kama Sudan au la.

Mwandishi, Tufail Hussain, ni Mkurugenzi wa Islamic Relief UK. Ana karibia miongo miwili ya uzoefu katika sekta ya kibinadamu, inayoongoza ukuaji wa mageuzi, kutetea uwezeshaji wa vijana, na kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu majanga ya kibinadamu.

Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayaakisi maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.

TRT Afrika