Na Sylvia Chebet
Machafuko ya raia iliyosababishwa na Mswada wa Fedha wa Kenya 2024 huenda ikawa imekadiriwa vibaya, hata hivyo imeacha hali ya kutokua na utulivu wa kudumu kwa taifa hilo la Afrika Mashariki kukabiliana nayo.
Uamuzi wa serikali ya Rais William Ruto kukubali matakwa ya waandamanaji wanaopinga ushuru umesababisha mashirika matatu makubwa ya kimataifa ya kutathmini viwango vya mikopo kushusha hadhi ya Kenya kutoka B hadi B-.
Ushushaji hadhi wa hivi punde ulitoka kwa 'S&P' mnamo Agosti 23, na kuisukuma zaidi katika eneo ambalo soko la mikopo huita "junk".
"Kupunguzwa kwa kiwango hicho kunaonyesha maoni yetu kwamba mtazamo wa fedha wa muda wa kati wa Kenya na madeni utadorora kufuatia uamuzi wa serikali wa kubatilisha hatua zote za ushuru zilizopendekezwa chini ya Mswada wa Fedha wa 2024/2025," shirika la ukadiriaji la Marekani lilisema.
Raymond Gilpin, mwanauchumi mkuu wa Afŕika katika Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), anabainisha kuwa madhaŕa ya upunguzaji wa haŕaka ya mikopo hayatoathiri tu seŕikali lakini pia na mwananchi wa kawaida.
"Kiwango cha riba ambayo Kenya inalipa kwenye deni lake huenda ikaongezeka. Wale wanaoikopesha nchi bila shaka wataona kama kuwepo kwa uwezekano wa hatari ya kutolipa deni zaidi na hivyo basi, viwango vya riba kwenye bondi au mikopo ambayo haijarekebishwa vinaweza kupanda," anaiambia TRT Afrika.
Viwango vya riba vinapoongezeka, mara nyingi zaidi husababisha athari kwengineko, ikiwa ni pamoja na ongezeko kubwa la gharama ya bidhaa na huduma.
Wanauchumi wana wasiwasi zaidi kuwa kuongezeka kwa gharama ya deni kunaweza kupunguza uwezo wa serikali wa uwekezaji haswa katika kutengeneza ajira na sekta za kijamii kama vile afya na elimu.
"Takwimu zinaonyesha kuwa Waafrika milioni 750 wanaishi katika nchi zinazolipa deni kuliko kile wanachowekeza katika afya na elimu," anasema Gilpin.
Jinsi nchi zinavyotathminiwa
Wawekezaji na watoa deni hutegemea mashirika ya kukadiria mikopo kwa taarifa kuhusu athari zinazohusiana na mkopaji.
Tathmini za mikopo huwa muhimu hasa wakati mwekezaji wa nje hajafahamu muktadha wa nchi mahususi, jambo ambalo kwa kawaida huwa kweli katika masoko yanayoibuka na yanayoendelea.
UNDP inaangazia kwamba ukadiriaji huru wa mikopo uliotolewa na S&P, Moody's na Fitch ni muhimu katika kuwezesha nchi zinazoibuka na zinazoendelea kupata ufadhili wa kutosha ili kufikia malengo yao ya maendeleo.
“Maoni haya ni matokeo ya kuangalia takwimu za uchumi jumla, kitaasisi na utawala kwenye nchi mahususi na kupata maelezo kuhusu mikopo kutoka kwa taasisi na watu binafsi wanaofanya kazi ndani au pamoja na nchi,” anafafanua Gilpin.
Kwa hivyo, je, mfumo kama huo hauwezi kuwa na udanganyifu au ushawishi usiofaa?
Hivi majuzi UNDP ilichanganua ukadiriaji wa mikopo huru katika uchumi wa Afrika ili kuangalia kama kuna upendeleo na kukagua uhusiano kati ya ukadiriaji na mchakato wa maendeleo.
Utafiti huo uliondoa uwezekano wa upendeleo katika mchakato wa tathmini wa mikopo ya Afrika kwa sababu mbinu kama hiyo inatumika duniani kote, ingawa ulifichua "ubaguzi" katika namna ya kutathmini unaotekelezwa na mashirika matatu makuu ya ukadiriaji.
Ubaguzi wa gharama
Utafiti wa UNDP unaonyesha kuwa nchi zinazoendelea kiuchumi zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na kushuka kwa kasi kwa hivi karibuni kwa viwango vyao vya mikopo, na kusababisha gharama kubwa za kukopa na kuongezeka kwa hatari za uhimilivu wa deni.
Takriban asilimia 95 ya kushuka alama kumetokea katika nchi zinazoendelea, jambo ambalo UNDP inakubali kuwa limeathiri vibaya uwezo wao wa kuongeza mtaji mpya na kudumisha ahadi zilizowekwa.
Utafiti ulibaini kuwa ili kuwepo kwa haki, mashirika ya ukadiriaji wa mikopo yanahitaji kiasi kikubwa cha data na uwezo, mambo ambayo yanakosa haswa wakati wa kufanya kazi katika nchi nyingi za Afrika.
"Ikiwa hawana data, lazima watoe hukumu za kibinafsi," anasema Gilpin.
"Wakati sisi katika UNDP tulifanya utafiti kwa nchi 19 za Kiafrika ili kuona inagharimu kiasi gani utoaji wa hukumu za kibinafsi, gharama hiyo ilifikia dola bilioni 74. Hiyo ni zaidi ya kile ambacho bara zima la Afrika hupokea katika misaada kila mwaka."
Hii ni sawa na asilimia 80 ya mahitaji ya kila mwaka ya uwekezaji wa miundombinu barani Afrika, inayokadiriwa kuwa dola bilioni 93. Gharama ya dola bilioni 74.5 za Marekani ni mchanganyiko wa riba ya ziada inayotozwa kwa mikopo na ufadhili ambao nchi hizi 19 zimetabiri.
Hiki ni kidokezo tu, ikizingatiwa kuwa utafiti huo haukuhusisha zaidi ya nchi 30 za bara hilo.
"Hizi ni mada ambazo tunaweza kurekebisha, na lazima turekebishe," anasema Gilpin. "Tuna jukumu la kulinda mustakabali wetu wa kiuchumi."
UNDP inafanya kazi na mashirika mengine kadhaa ili kuongeza uwezo wa utafiti katika nchi za Afrika ili kuhakikisha kwamba michakato yao ya kutathmini mikopo ina lengo zaidi na haitegemei maoni kutoka kwa waandishi ambao hawaishi barani.
Gilpin anasisitiza kuwa ufichuzi ni muhimu. “Kama nchi inashushwa hadhi kwa sababu ya X au Y, nchi inahitaji kujua ili waweze kuifanyia kazi,” anasema.
Fursa ya kuanza upya
Nchini Kenya, utawala wa Rais Ruto bado unakabiliana na deni la dola bilioni 78 za Marekani, huku waziri wa fedha akionyesha mapema mwezi huu kwamba serikali inapanga kukusanya takriban dola bilioni 1.2 za Marekani kwa kurejesha ushuru ambao haukupendwa na watu wengi.
Ingawa uchumi unaweza kupiga hatua zaidi kwa sababu ya kushuka kwa viwango vya hivi karibuni vya mkopo, Gilpin anaona matarajio mazuri.
"Kupungua kunaweza kupendekeza kwamba gharama na kiasi cha uwekezaji kitaathiriwa, lakini pia naona kama fursa ya kuanza upya. Ni jambo zuri kwamba serikali ya Kenya inatazama upya mswada wa fedha - kuona kile ambacho kinaweza kuahirishwa na kukatwa ili kusawazisha bajeti," anaeleza.
“Huu si wakati wa kukata tamaa. Ni wakati wa kurekebisha usawa wa kimuundo katika uchumi wa Kenya."
'S&P' inaona kuwa mtazamo wa Kenya ni "imara" licha ya kushuka daraja, ikitaja "ukuaji mkubwa wa uchumi unaotarajiwa na kuendelea kupata ufadhili wa masharti nafuu kutoka nje".