Na
Sylvia Chebet
Mataifa manne ya Afrika - Niger, Rwanda, Senegal na Tanzania - yana mgombea kila mmoja katika kinyang'anyiro cha kuwa mkurugenzi wa kanda wa WHO Afrika, wadhifa ambao unaambatana na majukumu muhimu ya kukabiliana na changamoto nyingi za afya ya umma barani humo.
Yeyote kati ya hao wanne atakayechaguliwa kuwa mrithi wa aliye madarakani, Dk Matshidiso Moeti wa Botswana, katika kikao cha 74 cha WHO Afrika kuanzia Agosti 26 hadi 30 huko Brazzaville nchini Kongo atarithi kazi ngumu.
Afrika inakabiliana na dharura 100 za afya ya umma zisizo za kawaida kila mwaka na mifumo ya afya inayohitaji kuwa katika hali bora zaidi.
Maziko Matemba, mchambuzi wa huduma za afya, anaorodhesha mabadiliko ya hali ya hewa, upatikanaji mdogo wa huduma za afya, kupungua kwa usaidizi wa wafadhili, na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama sehemu za ziada za zinazoumiza mifumo ya afya ya umma ambayo tayari imeelemewa.
Wagombea wanne wa kiti cha mkurugenzi wa kanda - Dk Faustine Engelbert Ndugulile wa Tanzania, Dk Ibrahima Socé Fall wa Senegal, Dk Richard Mihigo kutoka Rwanda, na Dk Boureima Hama Sambo wa Niger - wote ni wanakampeni wazoefu wa matibabu wanaofahamu kile wanachokitafuta.
Kiongozi mpya wa WHO Afrika anatarajiwa kuweka mifumo ambayo itafanya mamlaka ya afya ya kikanda kuitikia zaidi mahitaji ya nchi wanachama na kuwa na hamu ya kufanya kazi na serikali kwa ajili ya Afrika yenye afya bora.
"Huu ni msimamo ambao unaunda sera zinazosimamia usimamizi wa mifumo ya afya ya umma barani Afrika," Matemba anaiambia TRT Afrika.
"Tunatumai serikali na washikadau watamchagua mgombea bora zaidi, mtu ambaye anaelewa mifumo ya afya ya bara na anaweza kufanya kazi na serikali na watendaji wasio wa serikali, ikiwa ni pamoja na mashirika ya kiraia na sekta ya kibinafsi, kufikia huduma ya afya kwa wote ifikapo 2030."
Kufuatilia malengo muhimu ya afya
Kila mmoja wa wagombea hao amewasilisha mapendekezo kadhaa ambayo wanaahidi yataboresha utoaji wa huduma za afya chini ya mwongozo wa WHO Afrika ikiwa watapewa nafasi ya kuongoza afisi ya shirika hilo.
Akiwa daktari, mwanasiasa na mfuasi wa teknokrasia, Ndugulile anaamini analeta kila kitu kinachohitajika kwa kazi hiyo mezani.
Huku ikiwa imesalia miaka sita tu kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa ya "Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030", Ndugulile anasema kuwa nchi nyingi bado hazijafikia malengo yanayohusiana na afya. Mbaya zaidi, wakati bara linapambana na vitisho vya afya ya umma, baadhi ya vitengo vimeanza kutilia shaka umuhimu wa shirika la WHO.
"Tunahitaji kuwajibika kwa mahitaji ya nchi wanachama. Tunahitaji kuwa wastadi wa kupeleka ajenda ya afya ya Afrika katika jukwaa la kimataifa. Tunahitaji pia kushirikiana na wanasiasa na watunga sera katika bara la Afrika, watu wanaofanya maamuzi juu ya bajeti na utoaji wa huduma za afya,” anasema.
Ndugulile, mbunge anayehudumu katika nchi yake ya asili ya Tanzania, anatetea kile anachokiita "uongozi wa mabadiliko ya afya" ikiwa tunantaka athari za WHO Afrika kuonekana katika bara.
Mwenzake wa Senegal, Fall, alipata uzoefu wake wa kwanza wa kushughulikia dharura ya afya ya umma mwaka 1996 wakati mlipuko wa homa ya uti wa mgongo katika Sahel ulipoua watu 30,000.
"Niligundua kuwa afya ya kweli ya umma si kutibu magonjwa pekee. Kuelewa vigezo vya kijamii vya afya na kushughulikia mambo mapana huchangia ustawi wa umma," anasema.
Fall anapendekeza mfumo wa afya unazozingatia jamii, utamaduni na ushirikishwaji ili uwe na ufanisi.
"Tunahitaji kuweka afya katika msingi wa maamuzi ya kisiasa na kuhakikisha ufadhili wa kutosha kwa hilo," anasema Fall, mkurugenzi wa sasa wa Mpango wa shirika la WHO wa Magonjwa ya Kitropiki Yanayopuuzwa.
Mihigo wa Rwanda, ambaye amehusishwa na WHO kwa miaka 18 na kuhudumu kama kiongozi wa kimataifa wa Vaccine Alliance Gavi na mkurugenzi mkuu wa utoaji wa chanjo ya Covid-19, anasema Afrika haiwezi kumudu "kungoja kuokolewa na wengine".
“Maono yangu ni kuwezesha eneo letu kuweka afya katika kiini cha ajenda yake ya maendeleo zaidi,” anasema.
Sambo wa Niger, ambaye pia amehudumu katika nyadhifa mbalimbali ndani ya WHO tangu 2007, ni daktari anayezingatia magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
"Baada ya kufanya kazi katika kanda ya Afrika, nimekuwa na uzoefu wa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza na mapungufu ya mifumo ya afya. Tunahitaji kupambana na hali ya kutokwua na usawa katika sekta ya afya," anasema.
Kwa wagombea wote wanne, sehemu moja ya kipaumbele ya ni pamoja na kuongeza kasi ya huduma ya afya kwa wote kupitia huduma dhabiti za afya ya msingi, kuongeza ufahamu, na kuzuia magonjwa kwa umakini maalum wa kujiandaa kwa dharura ya kiafya.
Udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza, kuzingatiwa pakubwa kwa afya ya akili na kupatikana kwa huduma za uzazi na watoto za kutosha.
Huku kamati ya kanda ya Afrika ya WHO ikikutana Brazzaville baadaye mwezi huu kuteua kiongozi mpya, ahadi ya kufanya mabadiliko lazima yatimie.
Mustakabali wa afya ya Afrika na ufanisi wa mifumo yake ya utoaji wa huduma za afya uko hatarini huku wagombeaji wanne wakiahidi kufanya lile waezalo kwenye kazi yenye changamoto ya kutoa uongozi kwa bara katika nyanja ya afya.