Jeshi la Taifa la Uganda, UPDF limesema linafanya uchunguzi kubainisha sababau za mwanajeshi mmoja kujiuwa.
Luteni Among Ariho alikuwa katika kitengo cha uhandisi.
"Mkuu wa Majeshi anawahakikishia wananchi kwamba UPDF itafanya uchunguzi wa kina na yeyote atakayepatikana na hatia atafikishwa mahakamani," imesema taarifa iliyotolewa na jeshi la UPDF.
Tukio hili lilitokea Januari 2, 2024, mwendo wa saa nane mchana wakati Ariho aliposimamisha gari yake katika uwanja wa mpira, akawafukuza waliokuwepo hapo na baadaye akajipiga risasi kwa bunduki yake.
"Tunaelewa kwamba watu binafsi hawana ujuzi sawa au usawa wa kushughulikia changamoto, kwa hivyo tunawahimiza maafisa wetu kila wakati kutafuta usaidizi wa kitaalamu kwa kutumia mifumo yetu tuliyoanzisha," amesema Brigedia Jenerali Felix Kulayigye, Mkurugenzi wa Ulinzi wa Habari kwa Umma.
"Katika miaka ya hivi karibuni tumeona ongezeko la masuala ya afya ya akili miongoni mwa maafisa wetu. Tumejitahidi kutatua masula husika lakini ni wazi bado tuna kazi kubwa ya kufanya," Kanali Deo Akiiki, Naibu Afisa wa Ulinzi wa Habari kwa umma amesema.