Jeshi la Polisi Tanzania laimarisha ulinzi siku chache kabla ya maandamano

Jeshi la Polisi Tanzania laimarisha ulinzi siku chache kabla ya maandamano

Hatua hiyo inafuatia tamko lililotolewa na Chama cha CHADEMA la kuandamana siku ya Septemba 23, 2024.
Kikosi cha Kutuliza Ghasia nchini Tanzania./Picha: Reuters

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeimarisha ulinzi katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam, siku chache kabla maandamano ya chama cha upinzani cha CHADEMA.

Ulinzi huo umeimarishwa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, huku CHADEMA wakiwa wameazimia kufanya maandamano yao ya Septemba 23, 2024.

Magari ya Kikosi cha Kutulia Ghasia cha Jeshi la Polisi Tanzania, maarufu kama FFU yalionekana yakizunguka maeneo tofauti ya jiji hilo la kibiashara nchini Tanzania.

Chama hicho, pia kimeitaka serikali ya nchi hiyo kupitia Jeshi la Polisi Tanzania kuwarejesha viongozi wake ambao kinadai wametekwa na hawajulikani walipo, licha ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa amri kwa Jeshi hilo kuwatafuta.

“Tunawakaribisha wananchi wote wajitokeze kwa wingi tuandamane kwa amani na kufikisha maombolezo na kilio chetu ili kwa pamoja tuweze kukomesha mauaji haya ya kiholela nchini, hakuna ambaye yuko salama miongoni mwetu,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Afisa habari wa CHADEMA kwa kanda ya pwani, kama ilivyochapishwa kwenye ukurasa wa X wa chama hicho.

TRT Afrika