Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema kuwa limeanza uchunguzi wa taarifa za ‘kutekwa’ kwa Ally Mohamed Kibao ambaye ni Mjumbe wa Sekretarieti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Septemba 7, 2024, Jeshi hilo limesema kuwa limepata taarifa kuhusiana na tukio hilo kupitia vyombo vya habari vya nchini Tanzania kupitia kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.
“Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa kuwa, lilipokea taarifa hiyo na kuanza uchunguzi wa kubaini kilichotokea, chanzo chake na watu waliohusika ni akina nani,” alisema taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime.
Mapema siku hiyo, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika, alitangaza tukio la kutekwa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa ya chama hicho, Ally Mohamed Kibao.
Kulingana na Mnyika, tukio hilo lilitokea usiku wa Septemba 6, 2024, eneo la Kibo, karibu na Tegeta, wakati Kibao akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga kwa basi la Tashrif.
Akizungumza na wanahabari siku ya Septemba 7, 2024 Mnyika ameeleza kuwa basi hilo lilizuiwa na magari mawili ambayo hayakuwa na nembo yoyote na watu waliokuwa ndani ya magari hayo walikuwa na silaha.
"Walikwenda moja kwa moja kwenye kiti alichokaa Mzee Ally Mohamed Kibao, wakamchukua kwa nguvu na hata kumshambulia kabla ya kuondoka naye," alisema .