Baadhi ya Askari kutoka Jeshi la Polisi Tanzania./Picha: tanpol

Jeshi la Polisi Tanzania linatajwa kuwa moja ya taasisi bora zaidi barani Afrika, utafiti kutoka Shirika la Afrobarometer umeonesha.

Kulingana na ripoti iliyotolewa hivi karibuni na shirika hilo, Jeshi la Polisi la Tanzania ni kati ya taasisi zinazozingatia weledi na taaluma barani Afrika kwa sasa.

Wakati jeshi la Tanzania likiorodheshwa kuwa kati ya taasisi bora zaidi barani Afrika kiweledi, hali ni tofauti kwa majirani zao wa nchini Kenya ambapo jeshi la nchi hiyo limeorodheshwa kati ya taasisi zilizokosa weledi katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku.

Utafiti huo ambao ulifanywa kati ya mwaka 2021 na 2023 katika nchi 39 barani Afrika, linaangazia changamoto wanazokutana nazo raia wakati wa kufanya kazi na majeshi yao ya polisi.

Kulingana na utafiti huo, ni nchi tatu barani Afrika zilizojenga imani na majeshi yao ya polisi, kati ya 39 zilizojumuishwa kwenye matokeo ya utafiti huo.

Nchi zinazoshika nafasi za juu ni pamoja na Burkina Faso, Morocco na Benin, zikiwa na asilimia 68, 64 na 61 mtawalia, wakati Tanzania inashika nafasi ya tisa ikiwa na asilimia 53.

Kwa upande mwingine, nchi za Nigeria, Sierra Leone na Gabon zina majeshi ya polisi yasiyozingatia weledi katika taaluma hiyo.

Kulingana na utafiti wa Afrobarometer, taasisi hizo katika nchi tajwa zimeghubikwa na wimbi la vitendo vya rushwa na uonevu wa raia.

Kenya iko katika orodha hiyo, ikishika nafasi ya 10.

Wakati huo huo, ripoti hiyo imeanisha viwango vya imani kwa majeshi ya polisi barani Afrika, huku eneo la Afrika Kaskazini likiongoza kwa kuwa na asilimia 51 ya imani kwa taasisi hiyo, huku maeneo ya Mashariki na Magharibi yakigawana asilimia 50, wakati Afrika ya Kati ikiwa na kiwango cha chini kabisa cha asilimia 37.

TRT Afrika