Biashara ya kuuza majani ya muguka imestawi haswa katika pwani ya Kenya. /Picha: NTV

Na Mustafa Abdulkadir

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mapema wiki hii kaunti 3 za Pwani ya Kenya, zimepiga marufuku usafirishaji, uuzaji na utafunaji wa muguka. Kaunti hizo ni Mombasa, Kilifi na Taita Taveta. Hatua hio imezua hisia tofauti nchini Kenya haswa kutoka kaunti zinazozalisha mmea huo.

Hii inafuatia vilio vya muda mrefu kutoka kwa wakazi wa kaunti hizo pamoja na viongozi wa dini kwa magavana wao, wakitaka matumizi ya muguka yapigwe marufuku.

Baadhi ya wazazi hao, wamedai kwamba uraibu huo una madhara ya kiafya na ya kiakili, na kuongeza kuwa, unaharibu vijana na vizazi vijavyo. Baadhi ya wanawake nao, wamekuwa wakilalamika kwamba waume zao wameshindwa kuwajibika kutokana na uraibu huo.

Baadhi ya wazazi wamedai kwamba uraibu huo una madhara ya kiafya na kiakili. /Picha: Reuters

Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir amelaumu matumizi ya muguka kwa uharibifu mkubwa katika jamii ya watu wa Mombasa.

Gavana huyo amesema, "Taasisi zimethibitisha kuwa muguka imeacha uharibifu mkubwa sana kwa jamii, na ndio maana nimepiga marufuku uingizaji, uuzaji na matumuzi ya muguka Mombasa".

Aidha marufuko hiyo imepongezwa na baadhi ya watu na kukemewa na wengine. Wanaopeongeza hatua hiyo ni viongozi wa dini, wazazi na ndugu wa walioathirika na utafunaji wa muguka kwa njia moja au nyengine.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wa muguka na viongozi kutoka kaunti ya Embu ambayo ndio inaongoza kwa ukulima wa bidhaa hiyo wameilaani hatua hiyo na kusema kuwa itakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa nchi.

Wafanyabiashara wa muguka wameilaani hatua hiyo na kudai kuwa ina athiri uchumi wao.

Huku wakisema kuwa watapeleka kesi mahakamani, kupinga marufuku iliyowekwa na magavana hao kwa madai kwamba hawana mamlaka ya kutunga sheria kama hiyo.

Mwanasheria na mmoja na kiongozi wa upinzani Martha Karua, kupitia mtandao wa X, amedokeza kwamba katiba ya Kenya inahalalisha utumiaji wa miraa/mirungi na muguka.

Amesema marufuko hiyo ina utata, na kutaka kupatikane kwa suluhu ya haraka.

Ruto amesema nini?

Rais wa Kenya William Ruto akiwa kwenye shughuli ya kupanda mti nchini Kenya. /Picha: Wengine

Rais William Ruto baada ya kurudi kutoka Marekani ameahidi kutenga dola 3.7 katika bajeti ya mwaka huu ili kupanua uzalishaji wa miraa. Halikadhalika ametupilia mbali na kubatilsiha marufuku iliyowekwa na kaunti 3 za pwani za kuzuia utumiaji, uingizaji na uuzaji wa majani ya Muguka.

Rais Ruto amesema katika taarifa ya kwamba, ‘’Muguka inatambuliwa na sheria ya taifa, sheria nyingine zozote au amri zinazopingana na sheria ya kitaifa ni batili.’’

Na hivyo kufifisha matumaini ya wakazi wa Mombasa, Kilifi na Taita Taveta kuona uraibu huo ukipigwa marufuku.

Rais William Ruto pia amewasiliana na magavana wa kaunti hizo tatu na kutaka wakutane na Wizara ya Kilimo ili kujadili suala hilo.

Matamshi ya rais Ruto yameibua hisia kali miongoni mwa wakazi na viongozi wa kidini na kisiasa wa Pwani, wakisema sio lazima kuuzwa kwa muguka Mombasa au pwani kwa jumla, na mmea huo unaathiri afya na utendaji kazi wa vijana wao.

Pia wameghadhibishwa na mradi wa kuzinduliwa sehemu ya kutibu wagonjwa wa akili badala ya viwanda na vyuo vikuu vyenye kuleta manufaa kwa jamii.

Wameiomba serikali kutofananisha miraa na muguka, kwa sababu athari za muguka ni kubwa zaidi kwa afya na kusababisha madhara ya akili.

Si hilo tu, bali inapitkana kwa bei rahisi jambo ambalo linasabisha hata vijana wenye umri mdogo kushawishika kutumia. Wamesema hali ya vijana imezidi kudorora na mustakbali wao uko hatarini.

Gavana wa Kaunti ya Mombasa akitangaza marufuku ya uingizaji wa muguka Mombasa. /Picha: Citizen TV

Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Mombasa, Zamzam Mohamed, amesema, "Si sawa kwa wafanyabiashara wafaidike huku maisha ya watoto wao yakizidi kuharibika. Akisisitiza ya kwamba madaktari wamethitibitisha madhara ya muguka na hivyo wasilazimishwe kuitumia".

Mwaka 2019, aliyekuwa gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana ametoa hofu yake kuhusu madhara ya muguka na athari yake kwa vijana na kutaka ipigwe marufuku, kupitia makala ndefu kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Muguka ni nini?

Ni zao ambalo linatoka Mashariki mwa Kenya, Embu na huvunwa baada ya siku 7, tofauti na miraa ambayo huvunwa baada ya wiki nne.

Muguka inajumuisha viwango vya juu vya kemikali mbili za Cathines na Cathinones. Kemikali hizi zina vichangamsho vinavyoleta msisimko, uchangamfu, kuwa na aina ya furaha na wakati mwengine hata ya kupitiliza.

TRT Afrika