Na Dayo Yusuf
Uamuzi wa Kenya wa kuondoa marufuku ya miaka sita ya ukataji miti nchini humo umekuja huku kukiwa na mashaka kutoka kwa wanamazingira wanaoweka tahadhari iwapo kutakuwa na mafanikio na matokeo ya upandaji miti yaliyofanyika.
Wasiwasi zaidi unahusu iwapo eneo la kijani kibichi la taifa hilo la Afrika Mashariki lililokuwa limeachwa kama litakuwa limesheheni uoto wa Asili wa kutosha ili ukataji wa miti kuanza tena, au jinsi mamlaka inakusudia kufungua misitu.
"Kama tuanze kukata miti katika nchi hii, inapaswa kuanza kufanyika labda baada ya miaka 15 kutoka sasa, wakati miti ambayo tumepanda imekomaa vya kutosha, na tuna misitu mizuri zaidi," mwanamazingira George Mwaniki aliiambia TRT Afrika.
"Tuko chini ya kiwango cha miti kilichopendekezwa, na kwa kuzingatia hilo, tunapaswa kuhimiza upandaji zaidi na sio kukata miti," alishauri.
Zoezi hili la kuanza kwa ukataji miti limesikika sana baada ya Rais William Ruto alipotangaza kwa mara ya kwanza wakati wa ibada ya kanisa kwamba hatua ya serikali kuondoa marufuku ya kukata miti katika mashamba ya misitu iliyotangazwa kwenye gazeti la serikali itasaidia kubuni nafasi za kazi katika nchi inayozihitaji zaidi kuliko hapo awali.
"Hatuwezi kuwa na miti iliyokomaa inayooza msituni huku wenyeji wakiteseka kwa kukosa mbao. Huo ni upumbavu," Rais Ruto alisema. "Hii ndiyo sababu tumeamua kufungua misitu na kuvuna mbao - ili tuweze kutengeneza ajira kwa vijana wetu na kupanua biashara."
Wengi wanaona uamuzi huo kuwa kinyume na juhudi za nchi kukabiliana na ukataji miti. Wasiwasi mkubwa wa mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi John Kioli upo katika namna utekelezaji wake utafanyika.
"Nani atafuatilia ikiwa uvunaji wa miti unafanywa kwa njia inayotakiwa? Tutafuatiliaje miti iliyokatwa imekomaa? Mbona tunafungua misitu Yote kwa ajili ya kuruhusu zoezi hili?" alisema. "Ingekuwa ni hatua ya kimkakati kama tungejaribu hili katika kaunti moja kwanza kuona jinsi inavyofanya kazi.
Ikiwa mpango utafanya kazi, unaweza kufungua misitu katika maeneo mengine ya nchi." Mfumo katika kazi ya Idara ya huduma ya misitu nchini Kenya inayosimamia shughuli zote za misitu nchini imejitokeza kuunga mkono hatua hiyo ya Rais Ruto.
"Mpango wa kina wa usalama wa uvunaji juu ya upatikanaji, udhibiti na usimamizi wa uvunaji halisi na utoaji ripoti umewekwa," ilisema kwenye ukurasa wake wa Twitter wa Idara hiyo.
"Kama sehemu ya mpango, vyeti vya kupewa kibali huwasilishwa kwa wasimamizi wa vituo vya misitu kabla ya kuanza zoezi la uvunaji mbao." Shirika hilo lilisema litadhibiti wakati ambapo uvunaji unafanywa na unapoisha. "Baada ya kukamilika kwa ukataji na uondoaji wa vifaa, vibali vya kuondoka hutolewa kama ushahidi wa kufuata mahitaji yote."
Serikali pia inatarajia kukusanya ushuru kutokana na shughuli za ukataji miti. Kulingana na idara ya misitu, kuondolewa kwa marufuku ya kukata miti katika misitu iliyowekwa kwenye gazeti la serikali kulitokana na orodha ya mashamba yaliyokusanywa kupitia nyaraka za mashirika mengi.
Mwanamazingira Mwaniki anaona hii ni msumeno wa pande mbili. Kwa upande mmoja, Kenya inahitaji kukidhi mahitaji yake ya mbao ndani, huku kwa upande mwingine, inapaswa kuwa na tahadhari dhidi ya uharibifu wa mazingira.
"Nchi nyingi jirani hazina mashamba ya misitu.Hata hivyo, tunatumia fedha nyingi kila mwaka kununua kutoka kwao mbao zinazotolewa na misitu ya kiasili," alisema.
"Ukiitazama Afrika kwa ujumla, basi ni jambo la maana kwetu kukata mbao kutoka kwenye mashamba ya misitu hapa kuliko kuagiza nje, jambo ambalo lingetuokoa pesa nyingi. Lakini, kwa ujumla, ni wazo ambalo Sio zuri ikiwa utalichunguza kwa misingi ya misitu iliyopo nchini kwa sasa."
Mtaalamu mwingine wa mazingira, Dk John Recha, anasisitiza kuwa taasisi na wadau wote husika lazima washirikishwe katika mchakato huo ili kuepusha maafa yanayoweza kujitokeza
"Changamoto ya kuondoa zuio na marufuku ya kukata miti bila kuhusisha taasisi muhimu kama vile Huduma ya Misitu ya Kenya itakuwa kwamba wafanyabiashara wasio waaminifu watatumia fursa hiyo kuvuna miti na misitu iliyopo," aliiambia TRT Afrika.
Utafiti wa kihistoria wa misitu ya miinuko ya Kenya uliofanywa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), unaonyesha kuwa gharama ya kiuchumi ya ukataji miti katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki inazidi faida ya kitaifa kutokana na misitu na ukataji miti kwa uwiano wa 4:1
"Kupotea zaidi kwa miti na mimea mingine kutachangia sababu za ongezeko la joto, kuongezeka kwa hali ya jangwa, na matatizo kadhaa kwa wakazi wa kiasili." Kwa jumla, Pande zote mbili za mawazo zimewasilisha hoja halali iwapo tuendelee au tusiendelee na ukataji miti.
Huku Wakenya wakitafakari kitendawili cha kutafuta manufaa ya kiuchumi na kukata miti baada ya kusitishwa kwa miaka sita, wale ambao wanaona zoezi hili ni nyeti zaidi kwa mustakabali wa sayari hii wataendelea kushinikiza kupigwa marufuku kabisa kwa ukataji miti.
Lakini kuna uwezekano mkubwa wa washindi wa mjadala huu kuhimiza ukataji miti unaodhibitiwa kwani, kwa njia moja au nyingine, baadhi ya miti hii inaweza kuwa na nafasi ya kuokolewa isipotee.