Kenya inajiandaa na uzalishaji wa chanjo kati ya mwaka 2026 na 2027. / Picha: AP  

Na Sylvia Chebet

Janga la Uviko-19 lilikuwa ni zaidi ya tatizo la kiafya. Lilikuwa ni jukwaa la kujifunza , hususani kwa wale waliokumbwa na uhaba wa chanjo baada ya makampuni tofauti kusitisha uzalishaji wake.

Kenya ina nia ya kuondoa utegemezi wa aina hii, kutokana na uzoefu wa aina hiyo.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imejiunga na Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo (IVI) kama nchi mwanachama mwezi Juni, tukio ambalo Rais William Ruto amesifia hatua hiyo katika sekta ya afya.

Ruto, ambaye alipandisha barua ya Kenya katika hafla hiyo iliyofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Seoul, nchini Korea, na kusema Kenya itajifunza kutokana na changamoto ya kutafuta chanjo wakati janga hilo liliposhika kasi.

"Muda umefika kwa bara la Afrika kutambua umuhimu wa kujitegema katika sekta ya afya na kujitosheleza katika uzalishaji wa chanjo," alisema.

Waziri wa Afya wa Kenya, Susan Nakhumicha amesema kuwa hatua hiyo itaiwezesha nchi hiyo kuwa na ufanisi wa kutengeneza chanjo kwa bei nafuu.

"Mbali na hayo, Kenya pia itakuwa na uwezo wa kutoka kwenye utegemezi ," aliiambia TRT Afrika.

Uhamishaji wa teknolojia

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imejiunga na Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo (IVI) kama nchi mwanachama mwezi Juni, tukio ambalo Rais William Ruto amesifia hatua hiyo katika sekta ya afya./Picha: Ikulu ya Nairobi

Kama nchi mwanachama, Kenya sasa ina ufikiaji wa mtandao mkubwa wa kimataifa wa IVI wa watengenezaji na inasimama kupata uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa wazalishaji wanaoheshimika.

Wakati wa hafla ya kuidhinishwa kwa mkataba wa IVI nchini, Rais Ruto alisisitiza haja ya kuwezesha upatikanaji wa chanjo kwa wote, bila kujali utaifa na hadhi.

"Katika uzalishaji na usambazaji wa chanjo, hakuna mtu aliye salama hadi kila mtu awe salama," alisema.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa IVI, Jerome Kim, alithibitisha dhamira ya shirika lake la kujenga mfumo ikolojia wa chanjo imara na endelevu ambao unakuza sayansi, kuzuia magonjwa na kuokoa maisha. "Tunapofikiria juu ya usalama wa chanjo, lazima iwe ya kukusudia, kuwezesha na kujumuisha," alisema.

Wizara ya afya inasema IVI itashirikiana na mshirika wake wa utengenezaji, Taasisi ya Kenya BioVax, na mshirika wa utafiti, KEMRI, ili kutimiza majukumu ya uchunguzi wa magonjwa, uhamisho wa teknolojia na kuongeza kasi.

Washirika hao watatu, pia wataratibu majaribio ya kitabibu, na kutoa msaada wa kiufundi kwa ajili ya Shirika la Afya Duniani na uuzwaji wa bidhaa hizo.

Rais Ruto aliitaka IVI kuendelea kuondoa mipaka ya uvumbuzi ili kuimarisha juhudi za utafiti na maendeleo ya bara hili na kujenga mifumo thabiti ya afya.

Chanjo lengwa

Licha ya uwezo huo, Waziri wa Afya wa Kenya ana imani kuwa nchi hiyo itakuwa imejitayarisha vyema kwa mlipuko ujao wa magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Chanjo dhidi ya kipindupindu, surua, rubela na homa ya matumbo ni miongoni mwa magonjwa yanayolengwa katika uzalishaji huo.

"Hii itaimarisha utoaji wa huduma ya afya ya msingi nchini Kenya na kusaidia kuzuia magonjwa," alisema Nakhumicha.

Hivi karibuni, watoto wachanga na watoto wakubwa nchini Kenya waliachwa wazi kufuatia uhaba wa chanjo muhimu nchini kote, ikiwa ni pamoja na surua, rubela, polio ya mdomo, pepopunda-diphtheria na BCG.

Hivi karibuni, Kenya imekumbwa na uhaba mkubwa wa chanjo. Picha: Wengine

Wizara ya afya ilisema tangu wakati huo imenunua chanjo za dharura zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 9.6 na inalenga kuzisambaza katika vituo vyote vya afya mwezi huu.

"Chanjo ni njia ya uhakika ya kuzuia magonjwana hilo linawezekana iwapo tutawekeza kwenye chanjo," alisema Nakhumicha.

Kitovu cha kanda

Kenya inalenga kuwa kitovu cha kanda kwa bidhaa za afya na teknolojia zake, hususani kwa watoto na wasichana wadogo.

Kulingana na makadirio ya Wizara ya afya, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinawasilisha soko kubwa la dozi zaidi ya milioni 150 kila mwaka.

Wataalamu wa afya wanatabiri ongezeko la kiwango cha uzazi cha zaidi ya asilimia 2.3 kwa mwaka.

Kenya inaanzisha kituo cha ukubwa wa kati cha kujaza na kumaliza katika BioVax, huku uzalishaji wa kwanza wa kibiashara ukitarajiwa kati ya 2026 na 2027.

Zaidi ya hayo, uzalishaji wa chanjo nchini humo utatoa uhakika wa ajira kwa wanasayansi, wasimamizi wa miradi, mafundi katika eneo la Kenya na Afrika kwa ujumla.

TRT Afrika