Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Lightness Mollel anajaza ndoo za maji tayari kuwabebesha punda wake wawili, baada ya kazi ya siku nzima.
Mkazi huyo wa kijiji cha Nadosoito kilichopo katika kata ya Muriet, chini ya Mlima Meru nchini Tanzania, anamiliki punda wawili, ambao huwatumia katika biashara yake ya kuuza mkaa.
Kama walivyo wanawake wengi kutoka jamii ya Kimaasai mkoani Arusha, Lightness husambaza mkaa kwa wateja wake maeneo mbalimbali ya mji huo, ambao pia husifika kwa biashara ya utalii, kwa kutumia wanyama hao.
“Hii imekuwa kama sehemu ya maisha yangu, kutwa nazunguka na punda wangu, tukivumilia jua na mvua, ili mradi mkono uende kinywani," anaiambia TRT Afrika.
Kwa siku ya kawaida, Lightness ana uhakika wa kupata hadi dola 11 ( Tsh. 30,000) kutokana na biashara yake ya kuuza mkaa wa rejareja.
"Hakika, hii ni biashara ninayoitegemea sana na imenisaida sana kuongeza kipato changu na cha familia yangu," anasema mama huyo wa watoto watatu.
Hata hivyo, mabadiliko ya hivi karibuni katika punda wake, yalimlazimu Lightness kusitisha kwa mda biashara yake.
Lightness anasema aligundua vidonda na makovu makubwa kwenye ngozi ya punda hao na kuamua kusimamisha shughuli ya kuuza mkaa kwa muda.
Jambo la Kawaida
Ni jambo la kawaida sana kukutana na kina mama wa Kimaasai wakiwa na punda waliobeba mizigo migongoni mwao, katika mitaa mbalimbali ya mji wa Arusha, Kaskazini mwa Tanzania.
Jina la Mzamiru Yassin sio geni kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania. Umahiri wake awapo uwanjani, ulimfanya apewe jina la 'Kiungo Punda.'
Na ndiyo halisi ya wanyama hawa.
Hata hivyo, wanyama hawa hupitia mateso makubwa na hupewa matunzo hafifu kutoka kwa wamiliki wao, licha ya umuhimu wao katika shughuli za kila siku.
"Bila shaka, punda anabakia kuwa mnyama muhimu sana kufugwa katika kaya yoyote, kwa bahati mbaya watu wengi wanaonekana kutotambua umuhimu wake," anapendekeza Livingstone Masija, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kulinda Wanyama cha Arusha (ASPA).
Kulingana na Masija, punda ni mnyama muhimu kwa familia zilizo na kipato cha chini, baada ya ng'ombe.
"Tumeona jinsi punda wanavyosaidia katika kazi za nyumbani za kila siku kama vile kubeba maji na kusukuma mikokoteni iliyojaa kuni, lakini umuhimu wao kwa kawaida hauzingatiwi," anaiambia TRT Afrika.
Biashara haramu ya ngozi
Licha ya umuhimu wao kwenye jamii za Kiafrika, punda wengi wamechinjwa kutokana na mahitaji makubwa ya ngozi zao.
Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya 'Donkey Sanctuary', punda milioni 5.9 huchinjwa kila mwaka ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya 'ejiao,' dawa ya kitamaduni ya Kichina, inayotengenezwa kwa ngozi za wanyama hao.
Inakadiriwa kuwa, idadi hiyo inaweza kufikia milioni 6.7 ifikapo 2027.
Viwanda vyenye kutengeneza 'Ejiao' vimeongezeka maradufu, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Kati ya 2013 na 2016, uzalishaji wa kila mwaka wa 'ejiao' uliongezeka kutoka tani 3,200 hadi 5,600, ambao ni sawa na ukuaji wa kila mwaka wa zaidi ya asilimia 20.
Taarifa mbalimbali, pia zimeonesha uzalishaji wa 'Ejiao' ukiongezeka kwa asilimia 160, kati ya 2016 na 2021.
"Nchi za Kiafrika na nyengine kutoka Amerika Kusini ziliathirika kwa kiasi kikubwa na biashara hii," Masija anaeleza.
Takwimu hizo za kutisha, ziliilazimu Umoja wa Afrika (AU) kupiga marufuku biashara ya ngozi ya punda.
Zuio hili lilitolewa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Umoja huo, uliofanyika Februari 17 hadi 18, 2024 mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
'Tandiko Maalumu la Mgongoni'
Kulingana na Masija, taasisi imeanzisha michakato ya kuwalinda na kuwatunza punda, ikiwemo kuwaekea tandiko maalumu mgongoni.
"Tumekuwa tukiendesha jitihada za kuwatunza na kuwalinda wanyama hawa," anaweka wazi.
Taasisi hiyo imetoa mafunzo kwa wamiliki wa punda kama Lightness, ya namna ya kutengeneza matandiko hayo, kwa lengo la kuwakinga wanyama hao dhidi ya majeraha wanayopata kutokana na mizigo mikubwa wanayobeba.
Kulingana na Masija, mnyama huyo ni muhimu kwa maisha ya kila siku nchini Tanzania, hasa kwa wanawake wanaowategemea kwa kazi mbalimbali.
Idadi ya punda nchini Tanzania inakadiriwa kuwa 600,000, ingawa idadi hii inaweza kutofautiana kutokana na ufugaji na mambo mengine.
Mara nyingi, mizigo hiyo husugua sehemu ya mgongoni mwa punda na hivyo kuwasababishia maumivu makali na wakati mwengine hata majeraha.
"Tumefundishwa namna ya kutengeza matandiko haya na tunafuraha sana kwani yametusaidia kuwalinda punda wetu," anasema Lightness, ambaye kwa sasa amekuwa ni balozi wa punda, katika kijiji chake.
Mbali na kuwatengenezea punda wake wawili, Lightness pia anauza matandiko hayo kwa bei ya dola 4 (Shilingi 10,000) kwa kila tandiko.
"Inatia moyo kuona namna jamii zetu zinavyofurahia mradi huu na kwa sasa hatuna wasiwasi tena kuhusu ustawi wa punda wetu," anaongeza.
Wanyama walio hatarini
Katika risala yake aliyoitoa wakati wa wiki ya punda Mei 17, 2024, mjini Dodoma nchini Tanzania, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa nchi hiyo Alexander Mnyeti, alionya kuwa punda wapo katika hatari ya kutoweka, iwapo mipango endelevu ya kumtunza mnyama huyo itakosekana.