Mahakama nchini Marekani imekataa mpango ambao ungeruhusu kampuni ya ndege ya Boeing kujibu shtaka la kula njama na kulipa faini kwa kuwahadaa wasimamizi wa Marekani kuhusu ndege ya 737 Max kabla ya ndege mbili kuanguka, na kuua watu 346.
Jaji Reed O’Connor huko Texas alisema kuwa utofauti, ujumuishaji na usawa au sera za serikalini na Boeing zinaweza kuleta changamoto ya ubaguzi wa rangi katika kuchagua afisa wa kusimamia utiifu wa Boeing na makubaliano yaliyopendekezwa baada ya ajali za Boeing Indonesia na Ethiopia.
Tarehe 10 Machi 2019, ndege ya Boeing 737 MAX 8 iliyokuwa ikitoka mji mku wa Ethiopia Addis Ababa kuelekea Nairobi Kenya, ilianguka dakika sita baada ya kupaa. Abiria wote 149 na wahudumu 8 wa ndege walipoteza maisha.
Tarehe 29 Oktoba 2018, ndege ya Boeing 737 MAX ikiwa na abiria 181 na wahudumu 8, ilianguka kwenye Bahari ya Java dakika 13 baada ya kupaa.
Makubaliano ya Boeing
Mwezi Juni 2024, Boeing iliamua kupendekeza kukubali shtaka la ulaghai kutokana na ajali mbili za ndege za 737 Max zilizoua watu 346, Indomesia na Ethiopia baada ya serikali kuamua kampuni hiyo ilikiuka makubaliano ambayo yameilinda dhidi ya kushtakiwa kwa zaidi ya miaka mitatu.
Waendesha mashtaka waliipa Boeing chaguo hilo la kuwasilisha ombi la hatia na kulipa faini kama sehemu ya hukumu yake au kukabiliwa na kesi ya uhalifu wa jinai ya kula njama ya kulaghai Marekani.
Mkataba huo wa ombi, ambao ulifaa kupata kibali cha jaji wa shirikisho kuanza kutekelezwa, unatoa wito kwa Boeing kulipa faini ya ziada ya $243.6 milioni.
Hiyo ndiyo pesa iliyotakiwa kulipwa chini ya suluhu ya 2021 ambayo Idara ya Haki ilisema kuwa kampuni hiyo ilikiuka.
Mfuatiliaji huru angetajwa kusimamia usalama na taratibu za ubora za Boeing kwa miaka mitatu. Mpango huo pia unahitaji Boeing kuwekeza angalau dola milioni 455 katika mipango yake ya kufuata usalama.
Lakini walioathiriwa katika ajali za Boeing walisema ilikuwa njia ya serikali na kampuni hiyo kukimbia lawama ya kuwa iliuwa watu kwa makosa yake.