Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limehimiza kusitishwa kwa mradi mkubwa wa mafuta wa Afrika Mashariki unaoongozwa na kampuni kubwa ya Ufaransa ya TotalEnergies, na kuonya juu ya athari mbaya kwa mazingira na jamii za wenyeji.
Kampuni ya TotalEnergies na Shirika la Mafuta la Kitaifa la China la Offshore walitia saini makubaliano ya dola bilioni 10 mwaka jana ili kupanua maeneo ya mafuta ya Uganda na kusafirisha mafuta ghafi kupitia bomba la urefu wa kilomita 1,445 hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) limekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wa haki na mashirika ya mazingira, na kukabiliwa na hatua za kisheria nchini Ufaransa na ukosoaji katika Bunge la Ulaya.
Mradi huo mkubwa utadhuru kwa njia isiyoweza kurekebishwa mifumo ya ikolojia dhaifu na baadhi ya watu 100,000 wanaotarajiwa kuhamishwa kutokana na maendeleo yake wametendewa vibaya, HRW ilisema Jumatatu.
Lakini TotalEnergies inasema waliofurushwa na mradi huo wamelipwa fidia ipasavyo kwa ardhi yao, huku hatua zikichukuliwa kulinda mazingira.
Familia zilizoathirika
Watafiti wa Human Rights Watch walifanya mahojiano zaidi ya 90 mwezi Machi na Aprili mwaka huu, ikiwa ni pamoja na familia 75 zilizohamishwa, ambao wengi wao walisema walipokea fidia iliyocheleweshwa au duni. Wengine waliiambia HRW walilazimishwa kuuza ardhi yao.
"EACOP imekuwa janga kwa makumi kwa maelfu ambao wamepoteza ardhi ambayo ilitoa chakula kwa familia zao na mapato ya kupeleka watoto wao shuleni, na ambao walipokea fidia kidogo kutoka kwa TotalEnergies," Felix Horne, mtafiti mkuu wa mazingira katika shirika la HRW alisema.
Wakulima waliiambia HRW waliingia katika madeni baada ya kusubiri muda mrefu kulipwa fidia zao, huku wanakampeni wakiandika kesi 37 ambapo watoto walidaiwa kulazimishwa kuacha shule kwa sababu familia zao hazingeweza kulipa karo.
Baadhi walitia saini mikataba ya fidia kwa Kiingereza, lugha ambayo hawakuweza kusoma, huku wengine wakidai kuwa, "uwepo wa maafisa wa serikali na usalama kwenye mikutano ya hadhara ulichangia hali ya vitisho", HRW ilisema.