Kamati ya Bunge ya Uganda ya Hesabu za Serikali ililiambia Bunge kuwa Taasisi ya Moyo ya Uganda, yaani Uganda Heart institute, ilifanya kazi kwa zaidi ya siku 1200 bila dawa muhimu kwa ajili ya matibabu ya moyo, hii ni kutokana na upungufu wa dawa unaoshuhudiwa.
Kamati hiyo pia iliongeza kusema kuwa katika Hospitali ya Butabika inayohusika na wagonjwa wa afya ya akili upungufu wa dawa umeshuhudiwa kwa muda wa siku 372.
Hii ilifuatia matokeo ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye alifichua kuwa mara kadhaa, vituo vya afya vilikuwa na upungufu wa dawa na kusababisha ukosefu wa huduma muhimu.
Changamoto hii pia iko katika vituo vyengine vya afya nchini.
"Hospitali ya Butabika ilikuwa na upungufu kati ya siku 64-372, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Lira kati ya siku 4-69, Arua RRH siku 28-182 wakati Taasisi ya Moyo ya Uganda ilipata upungufu wa zaidi ya siku 1,000," alibainisha Muwanga Kivumbi, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali.
"Dawa aina ya Digoxine Inj ya kusaidia wale wenye tatizo la moyo haikupatikana kwa siku 1,210, Atesonate Inj ya malaria kwa siku 440 na Oral Morphine dawa ya kupunguza joto kwa siku 174,” aliongezea.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo, wakuu wa hospitali hizo mara nyingi walihusisha tatizo hilo kutokana na kuchelewa kwa Mamlaka ya Taifa ya Dawa, NMS kuchelewa kuzileta, idadi kubwa ya wagonjwa, kutosekana kwa uwiano kati ya usambazaji na mahitaji ya NMS.
Pia wamelaumu mamlaka husika kuchelewa kutoa majibu kwa wakati, huku wakilaumu Wizara ya Afya, Bohari ya Taifa ya Dawa na pia uhaba wa bajeti ya kila mwaka kwa dawa na huduma maalumu.
Ripoti ilionyesha kuwa ingawa bajeti inayotarajiwa ya Hospitali ya Moroto ilikuwa shilingi bilioni 1.28 Bilioni, ni milioni 86 pekee zilizotengwa, wakati huko hospitali ya Fortportal RRH, ni shilingi bilioni 1.3 pekee zilizotengwa kwa ajili ya dawa kwa mwaka mzima.
"Upungufu wa dawa kutokana na dawa hizo kutofikishwa katika vituo vinavyohitajika sio tu unadhuru maisha ya wagonjwa wanaohitaji dawa kwani unawanyima kupata dawa muhimu, lakini pia unaondoa imani ya wagonjwa katika mfumo wa huduma za afya ya umma," Muwanga aliliambia Bunge.
"Hii inaweza kusababisha wagonjwa kutafuta huduma za afya zisizofaa au zisizoweza kumudu. Mamlaka ya Taifa ya Dawa, NMS ilishindwa kusambaza dawa zilizokosekana hasa zile za zaidi ya mwaka mmoja za hospitali ya Butabika yenye wagonjwa wa afya ya akili."
Amesema Mamlaka hiyo, NMS inapaswa kuwajibishwa na kukemewa na Katibu wa Hazina kwa kutowasilisha dawa muhimu, vifaa tiba na kupuuza mahitaji na ratiba za tathmini za hospitali.