Rais wa Kenya William Ruto na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Moussa Faki Mahamat wanahudhuria Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Septemba 5, 2023. REUTERS/Moniah Mwangi

Mkutano wa marais wa mabadiliko ya tabia nchi barani Afrika jijini Nairobi umeangazia viwango vya juu vya riba kutoka kwa taasisi za kimataifa za kifedha kama sababu kuu ya serikali kutokuwa na kasi ya kujikwamua kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.

"Nchi zetu nyingi zimeingia katika dhiki ya madeni kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa," Rais wa Kenya William Ruto amewaambia wajumbe wa mkutano wa marais unaofanyika Nairobi nchini Kenya.

"Na ndio maana tunahitaji mazungumzo ya wazi kabisa na tunasema hivi: Tunapataje ufadhili wa masharti nafuu, tutawezaje kulipa riba kama wengine wanavyolipa, tunaifanyaje Afrika isitoe riba mara tano zaidi?"

Wakati huo huo, bwana Ruto amesema kuwa mataifa yaliyoendelea ingawa athari zake ni kubwa lakini hayawajibiki. "Kama kungekuwa na kampuni inayokusanya takataka za kaboni duniani kote Afrika ingekuwa na hisa kubwa zaidi," anaeleza rais Ruto na kuendelea kusema, "Tatizo pekee ni kwamba wale wanaozalisha takataka wanakataa kulipa ada zao na kudai kuwa kampuni imeharibika,” "Hatuombi kupendelewa, hatuombi kutendewa tofauti, tunataka mfumo wa kifedha wa haki ambao unatoa usawa kwa kila mtu. Hilo si jambo gumu sana kuomba.”

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir akimkumbatia kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wakati wa Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Septemba 5, 2023. REUTERS/Monicah Mwangi

Kwa upande wake, Rwanda inasema inaweka mbele sekta yake ya kibinafsi kuwekeza katika nishati ya kijani na pia inaunga mkono mabadiliko katika usanifu wa kimataifa wa fedha.

“ Mabadiliko yoyote ya thamani ya mikakati ya fedha lazima yapendekeze marekebisho ya madeni na kupunguza viwango vya riba," Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema.

Wakuu wa nchi wanasema serikali yao inalazimishwa kutenga fedha za maendeleo ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

"Kila mwaka tunapata uharibifu na hasara nyingi kutokana na matetemeko ya ardhi, vimbunga vya kitropiki na tunapoteza kila mwaka takriban dola milioni 5.7," anasema Azali Assoumani, rais wa Comoro.

Kenya ambayo ni mwenyeji wa Kongamano la Mabadiliko ya Tabia nchi Afrika, imepoteza zaidi ya ng'ombe milioni 2.5 kutokana na ukame wa muda mrefu ambao umekumba pia baadhi ya nchi kama vile Ethiopia, Somalia na Djibouti.

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki akiwahutubia wajumbe wakati wa Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Septemba 5, 2023. REUTERS/Moniah Mwangi

Akihutubia wajumbe waliohudhuria mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres ameyataka mataifa yaliyoendelea kutimiza ahadi ya kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Akinwumi Adesina akihutubia wajumbe wakati wa Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Septemba 5, 2023. REUTERS/Moniah Mwangi

"Nchi zilizoendelea lazima ziwasilishe mikakati ya kuaminika ya kukabiliana na hali ya kifedha maradufu ifikapo 2025 kama hatua ya kwanza ya kutumia angalau nusu ya fedha zote za mabadiliko ya hali ya hewa ili kukabiliana na hali hiyo. Ni lazima pia watimize ahadi yao ya kutoa dola bilioni 100 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea kama msaada wa mabadiliko ya tabia nchi, na kujaza kikamilifu kopo la mipango ya kijani,” Guttieres amesema.

Viongozi hao pia wametambua kuwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi ni lazima yaongozwe na wanawake na vijana. Benki ya Maendeleo ya Afrika imetenga dola bilioni moja kwa ajili ya kufadhili uwekezaji wa vijana katika mabadiliko ya tabia nchi.

Barabara ya kijani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia wajumbe wakati wa Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Septemba 5, 2023. REUTERS/Monica Mwangi

Afrika inatazamia kupanga njia ya ukuaji wa kijani na nishati safi .

Huu ndiyo ujumbe wa viongozi wa Afrika katika mkutano wao wa Nairobi.

"Mkutano wa marais wa mabadiliko ya tabia nchi Afrika utaunda njia ya baadaye ya maendeleo ya hali ya hewa Afrika, tunakusanyika kwa sababu watu wa Afrika wanatutarajia kuchukua hatua," Akiwumni Adesina, rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika alisema.

Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia wajumbe wakati wa Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya, Septemba 5, 2023. REUTERS/Monica Mwangi

"Tunapokusanyika leo tukitega masikio vya kutosha, tutasikia wito wa dharura kutoka kwa wakulima ambao mazao na mifugo yao imeharibiwa, sauti za wavuvi ambao uvuvi wao unapungua, sauti za vijana ambao mustakabali wao unaendelea. kuathiriwa, sauti za wanawake na watoto wanaobeba mzigo mkubwa wa mabadiliko ya hali ya hewa,” Adesina anaongeza.

Viongozi hao wanatumai kuwa maazimio ya mkutano wa Nairobi yatatoa sauti kubwa ya Afrika huku bara linapojiandaa kwa mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi maarufu kama COP 28 utakaofanyika Dubai kuanzi tarehe 30 mwezi Novemba hadi 12 mwezi December mwaka 2023 huko Dubai.

TRT Afrika