Gavana wa jimbo la Kivu Kusini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesitisha shughuli zote za uchimbaji madini katika eneo hilo lenye machafuko na kuamuru makampuni na waendeshaji kuondoka katika maeneo ya uchimbaji madini, alisema Ijumaa.
Gavana Jean-Jacques Purusi Sadiki alisema katika taarifa yake kwamba kusimamishwa kazi hadi ilani nyingine kulitokana na "machafuko yaliyosababishwa na waendeshaji madini," bila kufafanua.
“Kampuni, wafanyabiashara na vyama vyote vya ushirika vinatakiwa kuondoka kwenye maeneo ya uendeshaji ndani ya saa 72,” alisema.
Uamuzi huo utawaathiri zaidi wachimbaji wadogo wa madini kama vile dhahabu na bati, kwa kuwa wao ndio wazalishaji wakuu wa eneo hilo.
Hata hivyo agizo lake hilo limezua shutuma kali kutoka kwa wadau wanaodai kuwa anakiuka mipaka yamadaraka yake.
"Uamuzi huo ni kinyume cha sheria na unaangukia katika wigo wa matumizi mabaya ya madaraka," alisema Jean Pierre Okenda, mchambuzi wa masuala ya utawala katika sekta ya uziduaji nchini Kongo, akiongeza kuwa waziri wa madini wa Congo anapaswa kuomba kwa haraka marufuku hiyo kuondolewa.
Katika taarifa tofauti, gavana huyo alitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa Julai 30 na waendeshaji madini ili kutathmini hali hiyo.