Gabon yenye ukubwa wa misitu inayokadiriwa kuwa asilimia 88 ilipokea dola za kimarekani milioni 17 kutoka kwa Mpango wa Utunzaji wa Misitu Afrika ya Kati (CAFI), ambayo ni programu ya Umoja wa Mataifa (UN), inayokusudia kupunguza gesi ya carbon hewani kupitia utunzaji wa misitu.
Hatua hii ilipelekea Mji mkuu wa Gabon, Libreville kuwa mwenyeji wa Kongamano la ‘African Climate Week’ kati ya Agosti 29 na Septemba 2 mwaka huo wa 2021. Kongamano hilo muhimu liliwaleta pamoja viongozi na washikadau tofauti wa mazingira, kujadili mustakabali wa Afrika kuelekea mkutano wa COP27, ambao uliratibiwa kufanyika mwezi Novemba.
Fursa kiuchumi - dola bilioni 2
Kwa mujibu wa Serikali ya Gabon, ongezeko la joto duniani pamoja na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla wake zinatokana na mataifa yanayochukulia suala la utunzaji wa mazingira kwa wepesi.
Taifa hilo ambalo limetwikwa jina ‘pafu la pili la dunia’ kutokana na utunzaji wake wa mazingira linasadiki kuwa linapaswa kutuzwa zaidi kutokana na mikakati yake madhubuti ya kupunguza gesi ya carbon hewani.
Mwana-mazingira Lee White ambaye pia ni Waziri wa maji na mazingira nchini Gabon anasema kuwa taifa hilo linakusudia “kuvuna misitu yake kwa mbinu endelevu ili kuzalisha mapato.”
Mpango wa ‘carbon credits’
Mchakato wa kupunguza gesi ya carbon hewani hutegemea pakubwa utunzaji wa misitu kwa kuzuia ukataji miti kiholela. Mbinu hii inayopigiwa upato sana na Umoja wa Mataifa inatoa nafasi nzuri kwa taifa la Gabon kufanikisha ‘carbon credits,’ ambayo ni chanzo bora zaidi cha mapato kuliko unyonyaji misitu kwa ajili ya kilimo.
Mataifa ya bara la ulaya ni sharti pia yazingatie kiwango cha mwisho cha utoaji wa gesi ya carbon hewani; kwa mfano nchini Ufaransa kiwango cha mwisho cha utoaji carbon kilikuwa ni tani milioni 450 mwaka 2020. Iwapo nchi au kampuni itatoa gesi ya carbon inayozidi kiwango cha mwisho walichowekewa, basi italazimika kununua ‘carbon credits’ kufidia upitilizaji na ukiukaji huo.
Libreville inataka kubuni ‘carbon credits’ milioni 187 huku ikitarajiwa kuwa ‘carbon credit’ moja itakuwa ni sawa na tani moja ya gesi ya carbon --- ambayo wanapanga kuuza nusu yake na kuzalisha dola bilioni mbili.
Gabon vilevile iko kwenye hatua za mwisho za kutunga sheria kuhusu usimamizi wa mapato yatokanayo na uuzaji wa ‘carbon credits.’ Inatarajiwa kuwa asilimia 35 ya mapato yatawekezwa kwenye ulindaji na utunzaji wa misitu, asilimia 15 kusaidia jamii vijijini huku asilimia 50 zikielekezwa kwenye huduma za mikopo na msaada wa bajeti.
Viumbe hai wa majini
Ili kufikia malengo yaliyowekwa ya kupigana na ongezeko la hali ya joto duniani, Serikali ya Gabon imeweka mikakati ikiwemo upandaji wa miti zaidi na ulindaji wa viumbe hai wa majini. Jumla ya hifadhi 20 za baharini zimewekwa huku wavuvi wakitakiwa kujiepusha na mbinu za uvuvi zisizo endelevu.
Wanasayansi wanaeleza kuwa ulindaji wa bahari na viumbe hai wake huchangia pakubwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa mfano ni jambo lisilowezekana kuzuia miamba ya matumbawe na ongezeko la joto lakini kupunguza athari zitokanazo na ongezeko hilo inawezekana.
Kwa mfano zaidi ya asilimia 90 ya miamba ya matumbawe katika eneo la ulinzi la ‘Chagos Archipelago Marine’ ilikuwa imedidimia mwaka 1998 lakini ilipofikia 2010, ikaanza kurejea taratibu.
Ulindaji wa misitu na vita dhidi ya Uwindaji haramu
Serikali ya Gabon imebuni mbuga 13 za wanyama --- ambayo ni sawa na asilimia 11 ya ardhi ya nchi hiyo. Aidha Gabon iko makini sana kulinda viumbe vilivyo kwenye hatari ya kutoweka. Wanyama kama vile tembo na sokwe wanalindwa katika mbuga hizi 13 huku serikali ikiweka mikakati madhubuti ya kupigana na uwindaji haramu.
Juhudi zote hizi zimechochea mabadiliko mengi; kwa mfano idadi ya tembo iliyokuwa imefeli kwa asilimia 86 ndani ya kipindi cha miaka 30 sasa imeongezeka maradufu ndani ya miaka kumi.
Hatahivyo kumeshuhudiwa manung’uniko si haba miongoni mwa jamii zinazoishia karibu na misitu kuwa wanyama wanaharibu chakula chao shambani lakini serikali imeweka bayana kuwa changamoto hiyo inapaswa kushughulikiwa na vyombo husika vya serikali na sio wananchi kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuwadhuru wanyama.