Baba wa raia wa Tanzania waliotekwa nyara alisema Jumanne kuwa anaomba kuwepo kwa suluhu huko Gaza wakati familia yake ikivumilia "usiku wa kutojua usingizi" ikisubiri habari.
Serikali ya Israeli imewataja Watanzania Joshua Loitu Mollel na Clemence Felix Mtenga kama miongoni mwa takribani watu 240 waliotekwa nyara katika uvamizi wao wa kutisha wa Oktoba 7 Israel.
Wawili hao walikuwa nchini kwa mpango wa mafunzo ya kilimo, serikali ya Israeli ilisema kwenye X, iliyokuwa Twitter, Oktoba 29.
Serikali ya Tanzania bado haijathibitisha kama walitekwa nyara, ikisema tu kwamba raia wake wawili nchini Israel hawajulikani walipo.
Mwisho wa vita
"Ningependa kuona pande mbili zinazopigana zikikubaliana kumaliza vita na kuwaachilia mateka wote," alisema baba ya Joshua, Loitu Mollel, alipokuwa akizungumza na AFP kwa njia ya simu.
"Najisikia vibaya wakati wote kwa sababu mwanangu sio mpiganaji. Alikwenda kwa mafunzo lakini sasa yuko kwenye matatizo," aliongeza.
Mollel alisema mwanawe wa miaka 21 aliishi Nahal Oz, kibbutz iliyo karibu na Gaza ambayo ilikuwa moja ya maeneo yaliyoshambuliwa na kundi la wapiganaji wa Kipalestina.
Mzee huyo wa miaka 50 alisema alizungumza na mwanawe kwa mara ya mwisho jioni ya Oktoba 5, siku mbili tu kabla ya uvamizi wa Hamas.
Raia kuuwawa
Mamlaka za Israeli zinasema zaidi ya watu 1,400, wengi wao raia, waliuawa katika shambulio la Oktoba 7 kutoka Ukanda wa Gaza.
Kujibu, jeshi la Israeli limeishambulia Gaza, ambapo wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas inasema zaidi ya watu 8,500 wameuawa, wengi wao watoto.
"Nimekuwa nikikumbana na nyakati ngumu tangu wakati huo huku nikipitia usiku wa kutolala. Kama wazazi, tunapitia nyakati ngumu za kuishi bila dalili yoyote ya usalama wa mtoto wetu," Mollel alisema.
Mollel, ambaye ni mwalimu kwa taaluma na anafanya kazi kama afisa elimu katika mkoa wa kaskazini wa Manyara nchini Tanzania, alimuelezea mwanawe kama "mtulivu, mtiifu na makini" kuhusu kazi yake.
Joshua - mtoto wa kwanza kati ya watoto watano - alimaliza diploma yake katika masomo ya kilimo kutoka chuo kikuu katika mji wa mashariki mwa Tanzania wa Morogoro na kisha akaenda Israel mwezi Septemba.
Mafunzo Israel
Mollel alisema mara baada ya mafunzo ya kilimo nchini Israeli kukamilika, Joshua alitaka kujitafutia maisha yake katika kilimo kama mkulima au mtaalamu wa fani hiyo.
"Ndugu zangu na marafiki wamekuwa wakitufariji na tunawaomba waendelee kumuweka Joshua kwenye sala zao ili arudi nyumbani salama," alisema, na kuongeza kuwa serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya mawasiliano ya kawaida na familia hiyo.
Siku ya Alhamisi iliyopita, wizara ya mambo ya nje ilisema kuwa inafahamu kuhusu "raia wawili wa Tanzania waliopotea ambao ni kati ya wanafunzi 260 wa Tanzania wanaojifunza mbinu za kisasa za kilimo nchini Israeli".
"Serikali imekuwa ikifanya kazi na mamlaka husika na wadau wengine kubaini waliko na kuwaleta salama," ilisema kwenye taarifa.
"Hatua hizi zinaendelea na wizara ina mawasiliano ya kudumu na familia zao kuwajulisha juu ya juhudi hizi."
Mpaka sasa, Watanzania tisa wanaoishi Israeli wamerudi nyumbani kwa msaada wa serikali, ilisema.