Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa ( UN General Assembly, UNGA) unaofahamika kama mojawapo ya mikutano mikubwa zaidi ya kidiplomasia duniani, utaanza Jumanne mjini New York, Marekani.
Mkutano huu uhusisha Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la UN, ambao ni wakati wa viongozi wa dunia kutoa hotuba kuhusu masuala mbalimbali.
Mkutano huu hufanyika kila mwaka katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, ukiwaleta pamoja wakuu wa nchi na serikali za nchi wanachama. Utafanyika kuanzia Septemba 24-30.
Kikao cha 79 kitafunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na kuongozwa na Rais wa zamani wa Cameroon Philemon Yong.
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni nafasi inayopigiwa kura na wawakilishi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kila mwaka. Rais huyu ndiye mwenyekiti na afisa msimamizi wa Baraza Kuu.
Takriban viongozi 133 wa nchi na serikali, makamu watatu wa marais, manaibu waziri wakuu 80 na mawaziri 45 wanatarajiwa kuhudhuria.
Kiongozi wa kila nchi atatoa hotuba.
Katika utamaduni ambao umedumishwa tangu 1955, kiongozi wa Brazil atatoa hotuba ya kwanza.
Baada ya Brazil, nchi mwenyeji, Marekani, itachukua nafasi ya pili na baadaye wengine kufuata.
Kumbukumbu za mikutano ya baraza la UN
Viongozi wanatarajiwa kupunguza hotuba hadi dakika 15 na kugusa mada kuu.
Viongozi wengi kutozingatia mipaka ya muda, hata hivyo, kumesababisha nyakati za kukumbukwa.
Miongoni mwa viongozi wanaokumbukwa kwa kutumia muda mwingi ni pamoja na Fidel Castro aliyekuwa Rais wa Cuba ambae alizungumza kwa dakika 296, Mummar Gaddafi wa Libya nae alizungumza kwa dakika 100 .
Mikutano ya Baraza Kuu imefanyika tangu kuanzishwa mwaka 1946 ikiwa na wajumbe 51.
Wakati mwengine mashuhuri katika historia ya Baraza Kuu ni pale Rais wa zamani wa Umoja wa Kisovieti Nikita Khrushchev alipogonga meza kwa ngumi yake na kuigonga kwa kiatu chake baada ya kukasirika wakati wa hotuba ya Ufilipino mnamo 1960.
Hotuba ya Rais wa zamani wa Venezuela Hugo Chavez ya mwaka 2006 pia inarudiwa mara kwa mara, ambapo alimwita Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush, ambaye alizungumza siku moja kabla, "shetani."
Mnamo mwaka wa 2018, Waziri Mkuu wa wakati huo wa New Zealand, Jacinda Ardern alihudhuria Mkutano Mkuu na mtoto wake wa miezi 3.
Mwaka wa 2017 Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump katika hotuba yake alisema kwamba "angeiangamiza Korea Kaskazini," ikiwa ni lazima.
Hata hivyo, mara kwa mara kuna viongozi ambao hupitisha dakika 15 kwa kiasi kidogo na bado inakubalika.
Wakati wa changamoto duniani
Viongozi wa Umoja wa Mataifa wanakutana wakati ambapo idadi ya migogoro, na vita inaongezeka.
Kwa hivyo, idadi ya migogoro kutoka Gaza hadi Ukraine, na kutoka Sudan hadi Haiti, inatarajiwa kuwa kwenye ajenda.
Inatarajiwa kwamba viongozi watazingatia Gaza, ambapo maafa yanaendelea kuripotiwa huku Israel ikiendeleza mashambulizi.
Huko Gaza, pamoja na kusisitiza usitishaji wa mapigano, nchi wanachama zinatarajiwa kuangazia ukiukaji wa Israel wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa, pamoja na ugumu wa kuwasilisha misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ameratibiwa kuhutubia asubuhi ya Septemba 26, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akipangwa mchana.
Mwaka huu, mada kuu ya majadiliano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni "Kutomwacha mtu nyuma: kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kuendeleza amani, maendeleo endelevu na utu wa binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo."
"Utaratibu wa kimataifa wa leo haufanyi kazi kwa kila mtu. Kwa kweli, ningeenda mbali zaidi na kusema: haifanyi kazi kwa mtu yeyote," Guterres alisema.
Mkutano wa kutaka mageuzi katika UN
Kwa hivyo, inatarajiwa kwamba viongozi watashughulikia mageuzi ya Baraza la Usalama na usanifu wa kifedha wa kimataifa.
Mkutano wa Kuzingatia Wakati Ujao" utafanyika kuanzia Septemba 22-23, kabla ya Mkutano Mkuu.
Utalenga kurekebisha taasisi za sasa za kimataifa kuendana na changamoto za sasa, wakati mkutano wa ngazi ya juu kuhusu kupanda kwa kina cha bahari utajadili mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Viongozi pia wanatarajiwa kufanya mashauriano kuhusu masuala mbalimbali kama vile malengo ya maendeleo endelevu, upinzani dhidi ya viini na upokonyaji wa silaha za nyuklia.