Wanajeshi wanane wa kikosi cha Monusco wakamatwa kwa madai ya unyanyasaji wa kingono . / Picha: AFP

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) umetangaza kuchukua "hatua kali" dhidi ya baadhi ya walinda amani wake wanaoshukiwa kuwa na "utovu mkubwa wa nidhamu,"

Kwa mujibu wa barua ya ndani ya ujumbe wa kulinda amani MONUSCO, iliyoonekana na Shirika la Habari la AFP, walinda amani 8 waliotumwa Beni, Mashariki mwa DR Kongo, walikamatwa Oktoba 1 huku afisa mmoja akisimamishwa kazi wiki moja baadaye kwa kuhusiana na madai ya unyanyasaji wa kijinsia na vurugu.

Walinzi hao wote ni katika kundi la Afrika Kusini la jeshi la Umoja wa Mataifa, na wanadaiwa kuhusika katika kile ambacho ripoti za ndani zinaelezea kama "ukiukaji wa utaratibu" wa sheria za Umoja wa Mataifa.

"Ofisi ya huduma za usimamizi wa ndani imearifiwa na hatua za tahadhari tayari zimechukuliwa kulingana na sera ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kutovumilia kabisa," MONUSCO ilisema katika taarifa iliyotumwa Jumatano.

Hatua ambazo zilichukuliwa "ni pamoja na kusimamishwa kazi, kuwekwa kizuizini na kufungwa kwa walinda amani waliohusika", jeshi la Umoja wa Mataifa lilisema, na kuongeza kuwa "inalaani vikali tabia kama hiyo, ambayo haifai kwa wafanyikazi wa umoja wa mataifa".

"Baa na madanguro yanayoitwa majina Soweto, Bloemfontein na Cape Town," baada ya miji ya Afrika Kusini, yameibuka karibu na kituo cha MONUSCO huko Mavivi, karibu na Beni, kulingana na mojawapo ya taarifa.

Kulingana na ripoti ya awali, afisa huyo. "aliwatisha kwa maneno wafanyakazi wa umoja wa mataifa" kufuatia kukamatwa kwa walinda amani.

Tangu mnamo Mei, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amekuwa akizitaka nchi za SADC (Jumuiya Ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika), pamoja na Afrika Kusini, kupelekwa nchini humo kusaidia jeshi la Kongo dhidi ya waasi wa M23, ambao wameteka maeneo makubwa ya mkoa wa Kivu kaskazini.

Serikali ya DRC pia imekuwa ikitaka kuondoka kwa "haraka" kwa jeshi la Umoja wa mataifa kuanzia Disemba, ikishutumu kuwa imeshindwa kukomesha vurugu za makundi yenye silaha licha ya uwepo wake wa miaka 25.

AFP