Umoja wa Mataifa, washirika na mamlaka zinahamasisha msaada wa haraka – ikiwa ni pamoja na chakula, makazi na maji – kwa watu walioathiriwa na mafuriko. / Picha: Reuters

Mvua kubwa inayotokana na El Nino, imeongezeka hasa katika majimbo ya Puntland, Galmudug, Kusini magharibi, Hirshabelle na katika maeneo kando ya mto Juba katika Jimbo la Jubaland.

Zaidi ya watu 706,100 wameathiriwa kwa muda, huku watu wapatao 113,690 wakihamishwa makwao japo kwa muda.

Maeneo ya Kusini Magharibi na Jubaland ndizo zilizoathirika zaidi, kwani inakadiriwa kuwa watu 268,243 na 268,365 wameathiriwa na mafuriko hayo.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya mafuriko ya ghafla iliyoandaliwa na ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu, OCHA, kwa kushirikiana na mashirika ya kibinadamu na mamlaka nchini Somalia, ikiangazia hali kuanzia tarehe 6 Novemba 2023.

Aidha, Serikali ya Somalia imetangaza hali ya dharura katika maeneo ambayo mvua kubwa inayoshuhudiwa kati ya Oktoba hadi Desemba, imesababisha mafuriko, kulingana na Shirika la usimamizi wa Majanga nchini Somalia (Sodma).

Mashirika ya FAO / SWALIM yameonya juu ya hatari kubwa ya mafuriko ya mito Juba na Shabelle, huku ikiomba uanzishaji wa mipango ya uokoaji na kuonya watu wanaoishi kando ya sehemu nzima ya mto Juba kusaka njia salama za kuhamia maeneo ya juu.

Mamlaka nchini Somalia, imetoa wito kwa Jamii ya wasomali, hasa jamii ya wafanyabiashara, kuwasaidia watu walioathirika na mafuriko hayo.

Serikali ya Somalia imetangaza hali ya dharura katika maeneo ambayo mvua ya msimu wa vuli (Oktoba hadi Disemba) imesababisha mafuriko, kulingana na Shirika la Usimamizi wa majanga nchini Somalia (Sodma).

Maafa nchini Kenya

Barabara pia zimeharibiwa huku mafuriko hayo pia yakikatiza umeme na mtandao.

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limethibitisha kuwa watu 15 wamefariki dunia tangu kuanza kwa mvua kubwa wiki iliyopita, huku maeneo mengi yakiathirika zaidi.

Aidha, barabara kuu ya Modogashe, inayounganisha miji ya Garissa na Wajir Kaskazini Mashariki mwa Kenya, iliyojengwa hivi karibuni imeharibiwa pakubwa na mvua hizo na kulemaza shughuli za usafiri.

Rais William Ruto anatarajiwa kuunda kamati ya pamoja ya kukabilina na athari za El-Nino itakayojumuisha wadau wa serikali kuu na kaunti itakayosimamiwa na Naibu rais Rais Rigathi Gachagua.

TRT Afrika na mashirika ya habari