Rais wa Kenya William Samoei Ruto akihutubia Kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Septemba 21, 2023. REUTERS/Brendan McDermid

Rais Ruto aliyasema yote haya akiongea wakati wa mkutano wa 78 wa Umoja wa Mataifa Mjini New York, Marekani siku ya Alhamisi.

"Tunaweza kukubaliana kabisa, bila hofu ya upinzani, kwamba ulimwengu unaelekea kwenye mwelekeo usiostahili kabisa. Ni wakati kama huu ambapo roho ya kuthibitisha ushirikiano wa kimataifa, hatua za pamoja za kimataifa, na umoja wa ulimwengu unahitajika zaidi na unapaswa kuwa jambo linalowezekana." aliongeza.

Rais Ruto anafuata orodha ya viongozi wengine wengi wa mataifa mbali mbali hivi karibuni ambao wamekuwa wakiongea kuhusu jukumu ambalo Umoja wa Mataifa unacheza katika kuhakikisha usalama sehemu kubwa ya ulimwengu kwa ujumla.

Mapema wiki hii, Rais Felix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda walizungumzia njia nyingi ambazo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijakidhi matarajio katika kushughulikia masuala ya Afrika na hali ya sasa ya mapinduzi.

Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan pia alichangia katika mjadala huo siku ya Jumanne akisema "Lazima turekebishe mara moja taasisi zilizo chini ya Umoja wa Mataifa zenye jukumu la kuhakikisha amani, usalama na ustawi wa dunia."

Majadala wa Usalama umekuwa wa maana sana katika mkutano wa 78 wa Umoja wa Mataifa mwaka huu na hali ya dunia na yanayoendelea Ukraine na nchi za Afrika Magharibi zinachangia zaidi katika mjadala mzima wa mikutano ya mwaka huu.

"Maendeleo Duni"

Rais wa Kenya pia alilaumu Umoja wa Mataifa kwa "maendeleo yasiyoridhisha na hatua ndogo za mabadiliko ya tabia nchi, katikati ya maendeleo ya teknolojia na utajiri mkubwa."

Ruto aliongeza kuwa "mashindano" haya "yametuacha katika hali ya kushindwa kuchukua hatua, tukiendelea kupitia moja ya nyakati zenye giza zaidi kama binadamu."

"Hii sio fursa kwa mwanachama yeyote wa Umoja wa Mataifa kuepuka, wakati wanapaswa kujitokeza kukabiliana na changamoto." alisema.

Rais wa Kenya pia alitaja kuwa kutofuatisha ahadi zao na viongozi wa ulimwengu kutaleta "mazingira ya kutokuaminiana kote."

Kutokuaminiana huko, alisema, imekuwa ikijitokeza kati ya kaskazini ya ulimwengu dhidi ya kusini, nchi zilizoendelea dhidi ya zinazoendelea, matajiri dhidi ya maskini, wavujaji dhidi ya waathirika, na wazalishaji wa hewa ukaa dhidi ya waathirika wa hewa ukaa.

Uanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina nchi wanachama watano ambazo ni wanachama wa kudumu na nchi wanachama kumi zisizo za kudumu zilizochaguliwa kwa kipindi cha miaka miwili na Baraza Kuu.

Nafasi kumi zisizo za kudumu hubadilika kati ya nchi wanachama zaidi ya 170.

Wanachama wa kudumu ni China, Ufaransa, Urusi, Marekani, na Uingereza. Wote hawa wanayo nguvu ya kupinga mambo, maana hatua yoyote ambayo mmoja wao anapinga haina nafasi ya kufanikiwa.

Afrika imekuwa ikipigania nafasi ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2005.

TRT Afrika