Umiliki wa silaha limekuwa jambo lenye kutatiza wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki./Picha: Wengine

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Novemba 2024, mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye na Hajj Obeid Lulate, walikamatwa jijini Nairobi nchini Kenya kwa tuhuma za ‘kumiliki bunduki’ kinyume na sheria.

Baada ya kusafirishwa hadi Kampala nchini Uganda, upande wa mashitaka ndani ya Mahakama ya kijeshi ulidai kuwa wawili hao walikutwa na bunduki zinazodaiwa kumilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Uganda (UPDF).

Kesi hiyo, ambayo imevuta hisia za wengi, hasa ukizingatia kuwa Besigye, ambaye amewahi kuwa daktari binafsi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda, amewahi kuwa mwanajeshi wa UPDF.

Suala la umiliki wa silaha limekuwa lenye kutatiza wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye./Picha: @toprise

Licha ya kutofahamika na wengi, zipo sheria na kanuni zenye kudhibiti matumizi ya silaha na bunduki katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Nchini Tanzania, bei ya silaha aina ya bunduki inakadiriwa kufikia hadi Dola za Kimarekani 600, kutegemeana na aina ya silaha.

Hata hivyo, kuna vigezo na masharti ambayo yanapaswa kufuatwa ili mtu aweze kuwa mmiliki halali wa bunduki hiyo.

Kulingana na Kifungu cha 11 cha Sheria ya Umiliki na Usimamizi wa Silaha na Bunduki , ya mwaka 2015, ni lazima kwa mtu yeyote anayeruhusiwa kumiliki silaha hiyo awe ametimiza miaka 25.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa silaha zinaangukia mikononi mwa watu wazima wenye uwezo wa kufanya maamuzi ya busara.

Kuna vigezo na masharti ambayo yanapaswa kufuatwa ili mtu aweze kuwa mmiliki halali wa bunduki hiyo./Picha: Wengine

Vilevile, ni lazima mmiliki huyo awe na cheti chenye kuthibitisha uwezo wa kutumia silaha hiyo.

Hicho kinakuwa kama kithibitisho cha uelewa wa matumizi ya kifaa hicho, kulingana na kifungu hicho cha sheria.

“Pia ni lazima uwe raia wa Tanzania au uwe na kibali cha ukaazi cha kudumu. Hii ina maana kwamba wageni hawawezi tu kuja na kuanza kumiliki silaha hapa nchini,” inasomeka sehemu ya Kifungu cha 11 cha Sheria ya Umiliki na Usimamizi wa Silaha, ya mwaka 2015 nchini Tanzania.

Ukiwa umeonesha nia ya kumiliki silaha au bunduki, unapaswa uende kituo cha polisi kilicho karibu nawe ukiwa na ombi lako na mara moja uchunguzi wa tabia zako unaanza ili iweze kuthibitika kama unastahili kumiliki silaha au la

Kati ya vigezo vingi, mojawapo ni kuwa mtu anayetegemea kumiliki bunduki, hapaswi kuwa na rekodi za uhalifu.

Itakupasa uwe na fomu yenye kuonesha nia ya kumiliki silaha, ambayo itapelekwa kwenye Serikali za Mitaa, Kamati ya Usalama ya Mtaa wako, ili ujadiliwe na kisha kwenda kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya ambapo wangezipitia nyaraka hizo kabla ya kupelekwa kwenye Kamati ya usalama ya Mkoani na hatimaye mwishoni zingepelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha eneo husika.

Afisa wa Jeshi la Polisi la Tanzania akionesha moja ya silaha zilizotumika katika matukio ya uhalifu./Picha: Wengine

“Ukiwa umeonesha nia ya kumiliki silaha au bunduki, unapaswa uende kituo cha polisi kilicho karibu nawe ukiwa na ombi lako na mara moja uchunguzi wa tabia zako unaanza ili iweze kuthibitika kama unastahili kumiliki silaha au la,” anasema mtaalamu wa masuala ya ulinzi na usalama ambaye hakutaka jina lake litajwe kutokana na kazi yake.

Anaongeza: Utaenda ulipohifadhi silaha yako ukiwa na leseni yako na pia kibali cha kununulia risasi na hivyo kukabidhiwa silaha yako na pia kuuziwa risasi kwa idadi iliyokubaliwa kwenye kibali.

Kati ya vigezo vingi, mojawapo ni kuwa mtu anayetegemea kumiliki bunduki, hapaswi kuwa na rekodi za uhalifu./Picha: @JamiiForums

Katika mahojiano yake na TRT Afrika, mtaalamu huyo anasisitiza kuwa ni muhimu kuweka wazi nia ya kumiliki silaha hiyo, iwe kwa kuwinda au hata kwa ulinzi binafsi wakati unapeleka ombi lako.

Kulingana na mtaalamu huyo, kila silaha ina matumizi yake.

“Raia wa kawaida hawezi kuruhusiwa kumiliki silaha kama SMG au LMG kwani hizi ni kwa matumizi ya majeshi tu,” anaeleza.

Silaha ambazo raia wa kawaida anaweza kumiliki, kulingana na mtaalamu huyo ni ‘Shotgun’, ‘Pistol’ na ‘rifle’ maarufu kama ‘gobole’ ambazo mara nyingi hutumika katika shughuli za uwindaji.

Aina za silaha hutegemea na aina za matumizi./Picha: tacticaldefencetz.com

Kwa nchi kama Tanzania, silaha hizi huuzwa na kusambazwa na viwanda viwili vikubwa maarufu nchini humo, Mzinga kilichopo mkoa wa Morogoro ambacho pia kipo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Tanganyika Arms.

Hata hivyo, ikiwa unamiliki silaha, itakupasa kila mwaka uwe unalipia ada ya umiliki wa kifaa hicho.

Kwa mfano, kwa Tanzania, ada ya kumiliki bastola ni Dola za Kimarekani 40, Bunduki ni Dola 20, Gobole (Dola 20) wakati riffle ni Dola 15.

Aina ya silaha itumikayo na wadunguaji./Picha: Wengine

Nchini Kenya, udhibiti wa matumizi ya silaha hufanywa na Bodi ya Leseni za Silaha.

Bodi hiyo huwajibikia na kufanya uchunguzi wa iwapo mwombaji wa silaha anazo sifa stahiki na sababu za kufanya hivyo.

“Mwombaji anapaswa kuwa na walau miaka 18 na kuendelea, awe na tabia njema, awe raia wa Kenya asiye na rekodi ya makosa yoyote ya kihalifu,” inasomeka sehemu ya vigezo vya umiliki wa silaha kama ulivyotolewa na bodi hiyo.

Baadhi ya silaha zikiwa zimesalimishwa nchini Kenya./Picha: @ADFmagazine

Kwa upande wa Uganda, Sheria ya Umiliki Silaha ya mwaka 1970 inaweka wazi kuwa mwombaji wa kifaa hicho anapaswa kuwa amefikisha umri wa miaka 25 na kuendelea, awe na uwezo wa kutumia silaha hiyo na awe mtu mwenye afya nzuri ya akili.

Zoezi la kuharibu silaha haramu nchini Kenya./Picha: @ajplus

Raia wa kawaida hawezi kuruhusiwa kumiliki silaha kama SMG au LMG kwani hizi ni kwa matumizi ya majeshi tu

TRT Afrika