Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa mamlaka ya Somalia inapaswa kuheshimiwa baada ya Ethiopia kutia saini mkataba wenye utata na Somaliland iliyojitangazia uhuru.
EU ilisema katika taarifa yake Jumanne kwamba "ingependa kukumbusha umuhimu wa kuheshimu umoja, mamlaka na uadilifu wa eneo la Jamhuri ya Shirikisho la Somalia kwa mujibu wa katiba yake, Mkataba wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. "
"Hii ni muhimu kwa amani na utulivu wa eneo zima la Pembe ya Afrika," taarifa kutoka kwa msemaji wa EU ilisema.
Somalia siku ya Jumanne ilikataa makubaliano baina ya Ethiopia na eneo lake lililojitenga la Somaliland kuiruhusu kutumia bandari kubwa yenye ufikiaji wa Bahari Nyekundu, ikisema makubaliano hayo hayana nguvu za kisheria.
Somalia, ambayo inaiona Somaliland kama sehemu ya ardhi yake, pia ilimuita balozi wake nchini Ethiopia kwa ajili ya kujadiliana kuhusu makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi siku ya Jumatatu.
Ethiopia ina idadi ya watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 120, na ndio nchi yenye watu wengi zaidi isiyo na bahari duniani. Kwa sasa inategemea nchi jirani ya Djibouti kwa biashara yake kubwa ya baharini.
'Uchokozi usiokubalika'
Makubaliano hayo yatairuhusu Ethiopia, kukodisha kilomita 20 kuzunguka bandari ya Berbera, ambayo iko kwenye Ghuba ya Aden na ufikiaji wa Bahari Nyekundu, kwa miaka 50 kwa jeshi lake la majini na malengo ya kibiashara.
Kwa upande wake, kiongozi wa Somaliland alisema Ethiopia itaitambua Somaliland kama taifa huru, na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo.
Hata hivyo, Somalia ilitaja makubaliano hayo kama "uchokozi" na kuapa kutetea eneo lake.
"Kama serikali, tumeshutumu na kukataa ukiukaji haramu wa Ethiopia katika mamlaka yetu ya kitaifa na uadilifu wa eneo," Mohamud alisema.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema bungeni kwamba "hakuna mtu aliye na mamlaka kutoa hata kipande cha Somalia" baada ya mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri uliosema kuwa makubaliano kati ya Ethiopia na Somaliland ni "uingiliaji wa wazi wa uhuru, uhuru na umoja wa Somalia" na " batili na tupu".
Mohamud pia alisema: "Somaliland, ninyi ni mikoa ya kaskazini ya Somalia na Ethiopia haina utambulisho kwenu. Ikiwa Ethiopia ilidai ilikupa utambulisho, basi sio utambulisho wa ukweli."
Shrika la Reuters limemnukuu mshauri wa usalama wa taifa wa Abiy akisema kuwa Ethiopia itaipatia Somaliland hisa katika shirika la ndege la Ethiopian Airlines inayomilikiwa na serikali kama mrejesho kwa kuipa fursa ya kuingia kwenye Bahari Nyekundu. Haijulikani ni kiasi gani cha hisa.
Bado hakuna tamko la bainisho kutoka kwa serikali ya Ethiopia.
'Misri kutoa usalama'
Somaliland, nchi ambayo ilikuwa chini ya ulinzi wa Uingereza yenye takriban watu milioni 4.5, imekuwa ikitafuta utaifa kamili tangu ilipojitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991.
Lakini hatua hiyo haijatambuliwa kimataifa na inapingwa vikali na Mogadishu ingawa katika hali halisi, serikali kuu inatumia mamlaka kidogo juu ya masuala ya eneo hilo.
Huku kukiwa na mvutano katika eneo hilo, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Misri Abdel Fattah el Sisi siku ya Jumanne.
Urais wa Somalia ulisema viongozi hao wawili walisisitiza dhamira yao ya kuimarisha uhusiano na kusisitiza umuhimu wa kuunganisha juhudi za kushughulikia changamoto za pamoja katika kanda.
Sisi pia alithibitisha dhamira "isiyoyumba" ya Misri kusimama na Somalia na kutoa msaada kwa usalama na utulivu wake, kulingana na msemaji wa serikali ya Somalia Farhan Jimale.
'Somalia haiwezi kugawanywa'
Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita lakini haitambuliwi na Umoja wa Afrika au Umoja wa Mataifa kama taifa huru. Somalia bado inaichukulia Somaliland kuwa sehemu ya eneo lake na majibu ya maafisa kutoka huko yalikuwa ya haraka.
"Somalia haigawanyiki. Mamlaka yake na uadilifu wa eneo ni jambo lisilopingika,” Abdirizak Omar Mohamed, waziri wa petroli na rasilimali za madini wa Somalia, alisema.
Somalia ilichapisha kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii "X," zamani Twitter: "Ethiopia inajua vyema kwamba haiwezi kutia saini mkataba wa kijeshi/MOU ya kukodisha bandari na mkuu wa nchi wa eneo- mamlaka hayo ni haki ya Serikali ya Shirikisho ya Somalia.”
Somalia na Somaliland zilifikia makubaliano nchini Djibouti siku ya Ijumaa ili kuimarisha ushirikiano kuhusu usalama na mapambano dhidi ya uhalifu uliopangwa.
Ethiopia ilipoteza njia yake ya baharini wakati Eritrea ilipojitenga mwaka 1993. Ethiopia imekuwa ikitumia bandari hiyo katika nchi jirani ya Djibouti kwa uagizaji na usafirishaji wake mwingi.