Wizara ya Ulinzi ya Ethiopia Jumatatu ilikanusha taarifa za kuanguka kwa helikopta ya kijeshi katika mji wa kaskazini wa Bahir Dar.
"Hakuna uharibifu au ajali yoyote iliyohusisha helikopta ya Ethiopia," wizara ilisema katika taarifa.
Ripoti za Jumamosi zilidai kuwa helikopta ya Jeshi la Anga la Ethiopia ilianguka Bahir Dar.
Ripoti hizo hazikubainisha iwapo helikopta hiyo ilikuwa imebeba maafisa wa kijeshi au wawakilishi wa serikali, kwa mujibu wa Borkena News, chombo cha mtandaoni kilicho nje ya Ethiopia.
'Propaganda muflisi'
Hakukuwa na maelezo juu ya majeruhi au sababu ya tukio linalodaiwa.
Wizara ya Ulinzi ilitupilia mbali ripoti hizo, ikisema kwamba mkanganyiko huo ulitokana na kusimamishwa kwa muda kwa safari ya helikopta, ambayo baadhi ya wahusika walionyesha kwa uwongo kama ajali.
"Ripoti hizi si chochote zaidi ya propaganda muflisi za maadui wa Ethiopia," ilisema taarifa hiyo.
Vikosi vya serikali ya Ethiopia vimekuwa vikikabiliana na wanamgambo wa Fano, ambao wanajihusisha zaidi na eneo la Amhara.