Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed/ Picha: Wengine

Na Coletta Wanjohi

Mvutano unaongezeka katika Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo, IGAD, kwani baadhi ya nchi wanachama wake zinaonyesha waziwazi kutokua na imani na kambi hiyo ya kikanda.

IGAD inajumuisha Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda.

Wanachama wawili tayari wameweka wazi kwamba hawatahudhuria Mkutano wa Wakuu wa nchi uliopangwa kufanyika tarehe 18 Januari 2024. Inakusudiwa kutatua masuala ya msingi kati ya nchi wanachama.

Ethiopia imesema haitaweza kuhudhuria mkutano huo ikitaja kuwepo kwa masuala mengine ambayo yanaingiliana na mkutano uliopangwa.

Djibouti, mwenyekiti wa IGAD, ilitoa mualiko kwa wanachama wa IGAD wa Mkutano wa marais wa tarehe 11 Januari 2024.

Mualiko wake kwa nchi wanachama ulisema mkutano huo utakuwa juu ya "masuala mawili makuu ambayo ni masuala yanayoendelea kati ya Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na hali ya Jamhuri ya Sudan."

Mzozo wa Ethiopia na Somalia

Ethiopia kwa sasa iko kwenye mzozo na Somalia kuhusu mkataba mpya kati ya Ethiopia na Somaliland.

Ethiopia kwa sasa iko kwenye mzozo na Somalia kuhusu mkataba mpya kati ya Ethiopia na Somaliland.  /Picha:Ethiopia PMO

Tarehe 1 Januari 2023 Ethiopia iliandika makubaliano ya kukodisha ukanda wa pwani kutoka Somaliland kwa kubadilishana na kutambua mamlaka ya Somaliland.

Kama sehemu ya mpango huo, Somaliland inapanga kukodisha eneo la kilomita 20 (maili 12.4) kwenye ufuo wake hadi Ethiopia ili kuanzisha kituo cha jeshi la wanamaji, Rais wa eneo lililojitenga la Somaliland Muse Bihi Abdi alisema.

"Mkataba huo utafungua njia ya kutimiza matarajio ya Ethiopia kupata ufikiaji wa bahari na kupanua ufikiaji wa bandari za bahari," ilisema taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia.

Somalia, ambayo imesitisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Ethiopia imepinga mpango huo ikidai kuwa Somaliland haina uwezo wa kusaini mkataba huo, kwa sababu iko katika ardhi ya Somalia.

Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita lakini haitambuliwi na Umoja wa Afrika au Umoja wa Mataifa kama taifa huru. Somalia bado inaichukulia Somaliland kuwa sehemu ya eneo lake.

Rais wa Hassan Sheikh Mohamud amesema Ethiopai kufanya makubaliano na eneo la Somaliland ni uchokozi/ Picha: Wengine 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Somalia, Hamza Adan Haadow, anasema Somalia inapata nafuu kutokana na mzozo na haiwezi kumudu mgogoro mwengine na jirani.

Haadow alikuwa akizungumza na vyombo vya habari katika mji mkuu wa Uganda Kampala tarehe 17 Januari, kando ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Non Aligned Movement (NAM),

Somalia imetaka mkutano huu kuupa mzozo wake na Ethiopia kipaumbele.

Ethiopia inaonekana imedhamiria kuendelea na uhusiano na Somaliland.

Tayari wawili hao wametia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi.

Ethiopia, ambayo inashikilia nafasi ya Katibu Mtendaji katika uongozi wa IGAD, imesisistiza kuwa mkutano huo uliitishwa kwa "muda mfupi."

Marekani, ambayo ni ya hivi punde kutoa maoni yake kuhusu mzozo wa Somalia na Ethiopia, inasema mkataba mpya kati ya Ethiopia na Somaliland unaleta wasiwasi wa kiusalama.

"Tunachojali zaidi ni huu (Mkataba wa Maelewano) uliotiwa saini hivi karibuni kati ya Ethiopia na Somaliland unatishia kuvuruga mapambano ambayo Wasomali, Waafrika na washirika wa kimataifa wa kikanda, ikiwa ni pamoja na sisi, tunayoendesha dhidi ya Al-Shabab," John Kirby, mkurugenzi wa mawasiliano ya kimkakati wa Baraza la Usalama la Kitaifa amesema,

Sudan yakata uhusiano na IGAD

Sudan ni mwanachama mwingine wa kambi ya IGAD, pia imekaidi wito wa IGAD kujadili mzozo unaoendelea nchini mwake.

Majenerali Abdel Fattah al-Burhan na Mohammed Hamdan Dagalo wamezozana tangu Aprili 2023/ Picha Wengine

Mnamo Disemba 2023 Jenerali Abdel al Burhan, kiongozi wa Baraza Kuu, na pia kiongozi wa jeshi la Sudan na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, kiongozi wa Vikosi vya Rapid Support Forces walikubali kuanza mazungumzo ya kumaliza mzozo nchini mwao ulioanza Aprili 2023.

Hata hivyo, Sudan sasa imetangaza kwamba itasitisha ushirikiano wake na jumuiya ya kikanda ya IGAD.

Nchi hiyo ambayo imekuwa katika mzozo tangu Aprili 2023 inasema iliwekwa katika ajenda ya mkutano huo bila mashauriano.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilisema katika taarifa yake kwamba inapinga Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kualikwa kwenye mkutano huo pia.

Kukata uhusiano na IGAD kunamaanisha kukata juhudi za upatanishi ambazo jumuiya hiyo ya kikanda ilikuwa inafanya ili kutuliza nchi.

"Katika nyanja ya ushirikiano wa kimataifa, tofauti za asili katika nyadhifa na maslahi miongoni mwa nchi wanachama zinasisitiza umuhimu wa juhudi za ushirikiano katika kuunganisha mitazamo hii," Nuur Mohamud Sheekh, msemaji wa zamani wa Katibu Mtendaji wa IGAD amesema kwenye akaunti yake ya X.

"Mtazamo wa usalama wa leo unaenea zaidi ya mipaka ya kitaifa, ikijumuisha vipimo vya kikanda na kimataifa. Kwa kutambua mienendo inayobadilika, IGAD lazima ikubaliane na hali halisi hizi kupitia mashauriano jumuishi na mabadiliko muhimu ili kuimarisha ufanisi wake,” Sheekh ameongeza.

Nchini Sudan msimamo wa majenerali wa kutoafikiana haraka unaendelea kuwaathiri raia wake ambao hawajafurahia hali ya kawaida tangu kuondolewa kwa kiongozi wa zamani Omar El Bashir mwaka 2019.

Watu milioni 7.4 wamekimbia makazi yao ndani na katika nchi jirani kutokana na mzozo huo. / Picha:AFP

Zaidi ya miezi 9 ya mzozo huo ambao Umoja wa Mataifa unauelezea kama "mojawapo ya janga linalotokea kwa kasi ulimwenguni na janga kubwa zaidi la watu kuhamishwa ulimwenguni."

Takriban watu milioni 7.4 wamekimbia makazi yao ndani na katika nchi jirani kutokana na mzozo huo.

Matumaini ya uchaguzi kufanyika mwaka 2024 na mamlaka kuhamishwa kutoka kwa jeshi hadi kwa raia yanazidi kufifia, kuendelea kwa mapigano kati ya majenerali hao wawili kunafuta matumaini yoyote yaliyokuwa yamedumu.

"2024 inaitaka jumuiya ya kimataifa - hasa zile zenye ushawishi kwa pande zinazohusika katika mzozo nchini Sudan - kuchukua hatua madhubuti na za haraka kukomesha mapigano na kulinda operesheni za kibinadamu zinazokusudiwa kusaidia mamilioni ya raia," amesema Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu. kwa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura alisema mwanzoni mwa mwaka.

Hata hivyo, ikiwa makundi yanayopigana katika eneo la Pembe ya Afrika yanaepuka juhudi za kikanda za kutafuta amani basi wazo la kuwa na eneo lenye amani linaonekana kuwa mbali.

TRT Afrika