Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imeelezea wasiwasi wake juu ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais wa Senegal uliopangwa kufanyika hapo awali Februari 25.
Rais wa Senegal Macky Sall alitangaza kuahirisha kwa muda usiojulikana uchaguzi wa Jumamosi katika hotuba ya kitaifa, saa chache kabla ya kampeni rasmi kuanza.
Sall alisema alitia saini amri ya kukomesha hatua ya awali iliyoweka tarehe hiyo huku wabunge wakiwachunguza majaji wawili wa Baraza la Katiba ambao uadilifu wao katika mchakato wa uchaguzi umetiliwa shaka.
Hata hivyo, katika kuguswa kwake na maendeleo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, ilieleza kusikitishwa na mazingira yaliyosababisha kuahirishwa na kuzitaka ''mamlaka zenye uwezo kuharakisha michakato mbalimbali ili kupanga tarehe mpya ya uchaguzi. .''
Ukanda wa Afrika Magharibi umeshuhudia kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa tangu 2020 na mapinduzi kadhaa ya kijeshi na mgawanyiko mkubwa.
Wagombea wakuu wametengwa
ECOWAS imekuwa ikihangaika kusuluhisha mizozo kama hii huku Burkina Faso, Mali na Niger wakitangaza kujiondoa katika umoja huo wiki iliyopita. Nchi hizo tatu ambazo ziko chini ya utawala wa kijeshi kufuatia mapinduzi, zimeishutumu ECOWAS kwa kutowatendea haki.
Kuahirishwa kwa uchaguzi nchini Senegal kumezusha wasi wasi juu ya hali ya kisiasa nchini humo. Lakini ECOWAS imewataka wanasiasa kuendeleza mazungumzo katika kutatua hali hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa rais wa Senegal kuahirishwa.
Baraza la Katiba limewaondoa makumi ya wagombea kwenye kura hiyo, akiwemo kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko na Karim Wade, mtoto wa rais wa zamani Abdoulaye Wade. Hii imechochea hali ya kutoridhika inayoongezeka kuhusu mchakato wa uchaguzi.
Hakuna muhula wa tatu
Wagombea waliotengwa wanasema kanuni za kugombea hazikutumika kwa haki. Mamlaka zinakanusha hili. Lakini rais Sall alisema uchunguzi utafanywa kuhusu mazingira ya kutengwa.
"Hali hizi za kutatanisha zinaweza kudhoofisha uaminifu wa kura kwa kupanda mbegu za migogoro ya kabla na baada ya uchaguzi," Rais Sall alisema katika hotuba yake.
Amri ya Novemba 2023 iliyotiwa saini na Sall ilipanga uchaguzi huo kufanyika Februari 25, huku wagombea 20 wakiwa katika kinyang'anyiro hicho lakini bila viongozi wawili wakuu wa upinzani.
Sall alikuwa amesema mara kwa mara angekabidhi madaraka mapema mwezi wa Aprili kwa mshindi wa kura hiyo.
Baada ya kutangaza kuwa hatagombea muhula wa tatu kama rais, Sall alimteua Waziri Mkuu Amadou Ba kutoka chama chake kuwa mrithi wake.