Mahakama ya juu nchini Afrika Kusini, leo itatoa uamuzi juu ya rufaa iliyomnyima rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma kugombea tena nafasi ya uongozi wa juu wa Afrika Kusini.
Zuma, mwenye umri wa miaka 82, anakipigia chapuo chama kipya cha upinzani ambacho kinashiriki uchaguzi mkuu wa Mei 29.
Hata hivyo, mamlaka za uchaguzi za nchi hiyo zinasisitiza kuwa mwanasiasa huyo hana sifa za kugombea urais kwa madai kwamba alidharau maamuzi ya mahakama ya mwaka 2021.
Mahakama ya Katiba itatoa uamuzi baada ya hukumu ya awali ya mwezi Aprili kuwa upande wa Jacob Zuma.
Uchaguzi wenye ushindani mkubwa
Wataalamu wa sheria wanasema kuwa inaweza kuchukua siku chache kabla ya uamuzi huo kutoka.
Kesi hiyo inakuja majuma machache kabla ya nchi hiyo kuingia kwenye uchaguzi wenye ushindani mkubwa toka Afrika Kusini ilipopata uhuru wake mwaka 1994.
Hatua yake ya kuwekwa kifungoni mwaka 2021 iliibua machafuko makubwa nchini humo, yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 350.
Kuna hofu ya matukio hayo kujirudia.
Ni mahakama hiyo hiyo ambayo mwaka 2021 ilimhukumu Zuma kifungo cha miezi 15 jela baada ya kukataa kutoa ushahidi kwa jopo lililokuwa likichunguza tuhuma za ufisadi wa kifedha na ukaribu aliokuwa nao na familia ya Gupta wakati wa uongozi wake.
Na mkuu wa jopo hilo sasa ndiye jaji mkuu wa mahakama hiyo.