Licha ya AU kutambua Kiswahili kama lugha rasmi, Bado jumuiya ya Afrika Mashariki haijaidhinisha utumiaji wake kama lugha rasmi / Picha : X Jumuiya ya EAC 

Zaidi ya wataalamu 300 wa Kiswahili wamekusanyika mjini Mombasa kwa ajili ya kongamano la siku mbili la Kamisheni ya Kiswahili ya Kimataifa ya Afrika Mashariki lenye mada: Kiswahili, Elimu na wingi-lugha katika ufanikishaji wa Amani.

Kongamano hilo limeandaliwa chini ya mwamvuli wa jumuiya ya Afrika mashariki unaojumuisha mataifa ya Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Sudan Kusini na Somalia mbele ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani Julai 7.

Akizungumza wakati akifungua rasmi kongamano hilo Waziri wa Kenya wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi Aisha Jumwa amewataka wataalamu hao kuja na mapendekezo madhubuti yatakayowahimiza mawaziri wanaosimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwezesha kupitishwa kwa Kiswahili kuwa lugha rasmi. ya muungano huo.

“Lazima tutukuze Kiswahili. Kuzungumza Kiswahili si udhaifu utajiri wake unaonyesha umuhimu wake. Ikiwa wewe ni mzungumzaji wa Kiswahili kama mimi jivunie, si watu wote wana ujuzi na uwezo wa lugha ya Kiswahili,” akasema CS Jumwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Africa Mashariki , Veronica M. Nduva aliwataka wananchi wa jumuiy aya Afrika Mashariki kuipokea lugha hiyo kwa moyo wote akisema ndio ishara ya ushikamano wao.

''Kiswahili ni lugha yetu tunayoithamini sana na tunahitaji kuikumbati akwani ndio urithi wetu wa kitamadunina wenye kukuza umoja wetu,'' alisema Katibu Nduva katika video waliochapisha katika mtandao wa X.

Miongoni mwa ajenda katika kongamano hilo ni jinsi gani Kiswahili na elimu ya lugha nyingi inaweza kutumika kuelimisha jamii juu ya uimarishaji wa amani katika ngazi ya mashinani, kitaifa, kikanda na kimataifa.

"Ni lugha ambayo imeunganisha mataifa, jamii, tamaduni na kuimarisha umoja wetu kama Waafrika Mashariki," alisema Waziri Jumwa na kuongeza matumizi ya Kiswahili duniani kote ni ushahidi wa juhudi zinazofanywa na wadau.

Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) Nestor Kayobera alisema mkataba wa EAC unatambua lugha ya Kiingereza kuwa lugha rasmi lakini Kiswahili kinatambuliwa kama lugha iliyoenea kwa wengi lakini sio rasmi.

“Katika mkataba huo, Kiswahili ni lingua-franka lakini si lugha rasmi. Mkutano wa wakuu wa nchi za EAC ulijieleza kuwa Kifaransa na Kiswahili ni lugha rasmi, ni zaidi ya mwaka mmoja tangu mkataba huo haujafanyiwa marekebisho,” alieleza Jaji Kayobera.

Kiswahili ni mojawapo ya lugha zinazotumiwa sana katika familia za Kiafrika, na inayozungumzwa zaidi barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 230.

TRT Afrika