Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yameonya kuwa mapigano yanayoendelea Mashariki mwa DRC yanahatarisha kuzidisha mzozo wa kibinadamu katika eneo hilo, ambapo zaidi ya watu milioni 5 wamekimbia makazi yao katika majimbo manne.
Matumizi ya mizinga na makombora makubwa yamesababisha vifo vya watu kadhaa, na hospitali za Goma zimeshindwa kukabiliana na mmiminiko wa raia waliojeruhiwa.
Mgogoro unaoendelea kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, umetatiza usambazaji wa chakula katika mji wa mashariki wa Goma, na kuathiri zaidi ya wakazi milioni mbili na watu waliokimbia makazi yao.
Esperance Nyota, mkulima na muuza ndizi, alionya juu ya njaa inayokuja ikiwa mzozo utaendelea na njia zinazoisambaza Goma kutoka mashamba ya jirani kusalia kukatika.
"Mji mzima wa Goma unategemea soko hili dogo la usambazaji wa mihogo, mahindi na ndizi," Nyota alisema.
Takriban wakimbizi wa ndani 135,000 wamekimbia Sake katika wiki iliyopita, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi.
Wanaungana na mamia kwa maelfu ambao tayari wamekimbia makazi yao karibu na Goma tangu 2022 kutokana na mzozo unaoendelea.
Mapigano yameongezeka tangu kuanza kwa mwaka huu katika miji na vijiji vinavyozunguka mji mkuu wa mkoa huku waasi wakiteka eneo hilo na kuwalazimu maelfu kutafuta hifadhi katika mji huo.
Shirika la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba mzozo huo, ikiwa ni pamoja na utegaji wa mabomu kiholela, unahatarisha kuzidisha matatizo ya rasilimali chache za kuhudumia wakimbizi wa ndani zaidi ya 800,000, na milioni 2.5 ambao tayari wamekimbia makazi yao katika jimbo la Kivu Kaskazini.