Ramadhan Kibuga
TRT Afrika, Bujumbura, Burundi
Tume ya kitaifa ya Uchaguzi nchini DRC, CENI imetangaza usiku wa Jumamosi matokeo ya muda ya uchaguzi wa wabunge ikiwa ni majina ya wabunge 477 miongoni mwa wabunge 500 ambao watakaounda Bunge la Taifa.
Sehemu ambako uchaguzi wa wabunge wa mwezi Disemba ulifutiliwa mbali kutokana na dosari au haukufanywa kutokana na usalama mdogo watajazia baadae orodha ya wabunge waliosalia.
Kwenye matokeo hayo ya muda , orodha za wagombea wa Muungano wa Utawala''Union Sacree'' zimejiimarisha vizuri na hivyo kuashiria uwezekano wa wingi wa wabunge wanaomuunga mkono Rais Felix Tshisekedi.
Chama cha 'UDPS' cha Tshisekedi pekee yake kimeibuka nafasi ya kwanza na wabunge 69.
Aidha, sehemu kubwa ya washirika wa Rais Tshisekedi wakiwemo Wakuu wa Bunge na Seneti Christophe Mboso na Bahati Lukuebo, au pia Waziri Mkuu Sama Lukonde pamoja na manaibu Waziri Mkuu kama Vital Kamerhe, Jean Pierre Lihau na Christophe Lutundula wote wamechaguliwa katika ngome zao .
Vyama vyao au Muungano wa vyama wamerodheshwa miongoni mwa vyama vilivyopata kwa uchache asilimia 1 inayohitajika kisheria katika uwakilishi wa ubunge kwenye ngazi ya taifa.
'ACRN' na Dkt Mukwege watupwa nje.
Upande wa upinzani, Muungano wa Docter Denis Mukwege wa ACRN (Alliance pour la Refondation de la Nation) haukupata kiwango cha kura zinazohitajika. Hivyo hawatawakilishwa kwenye Bunge jipya.
Hata hivyo Chama cha 'Ensemble pour la République' cha mpinzani Moïse Katumbi watawakilishwa na kuwa chama muhimu cha upinzani. Licha ya kwamba baadhi ya vigogo wake hawakuchaguliwa kama wasemaji wake Herve Diakiese na Francis Kalombo
Haijajulikana msimamo wa Moïse Katumbi kuhusiana na matokeo haya. Awali alichagiza kuandaa upya uchaguzi.
Matokeo haya yamesalia kuwa ya muda.
Wanasiasa wana muda wa miezi miwili kufungua mashtaka mbele ya mahakama ya Katiba kuhusiana na migogoro ya kura kwa kusubiria maamuzi ya mwisho ifikapo tarehe 12 Machi 2024, kulingana na ratiba ya Tume ya Uchaguzi CENI.