Maafisa wawili wa polisi na mmoja wa washambuliaji waliuawa katika majibizano ya risasi yaliyoanza mwendo wa saa Kumi unusu asubuhi kwenye nyumba iliyoko Tshatshi Boulevard, kulingana na Muhima/ Picha :AP

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linasema "limezuia mapinduzi" mapema Jumapili asubuhi na kuwatia mbaroni wahalifu, wakiwemo raia kadhaa wa kigeni.

Taarifa ya shirika la AP inasema kuwa, watu watatu walifariki kufuatia ufyatulianaji wa risasi kati ya watu wenye silaha waliovalia sare za kijeshi na watu wanaoaminiwa kuwa walinzi wakuu wa mwanasiasa katika mji mkuu, Kinshasa.

''Jaribio la mapinduzi ya kijeshi lilichochewa na vikosi vya ulinzi na usalama vya Congo limetibuliwa na hali sasa imedhibitiwa," msemaji wa jeshi la Congo Brigedia Jenerali Sylvain Ekenge alisema katika mkutano na vyombo vya habari. Hakutoa maelezo zaidi.

Haya yanajiri huku kukiwa na mzozo unaokumba chama tawala cha Rais Felix Tshisekedi kuhusu uchaguzi wa uongozi wa bunge ambao ulipaswa kufanyika Jumamosi lakini ukaahirishwa.

''Watu hao waliokuwa na silaha walishambulia makazi ya Kinshasa ya Vital Kamerhe, mbunge wa shirikisho na mgombea wa spika wa Bunge la Kitaifa la Congo, lakini wakazuiwa na walinzi wake,'' Michel Moto Muhima, msemaji wake alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X.

''Mheshimiwa Vital Kamerhe na familia yake wako salama na wako salama. Usalama wao umeimarishwa,” Michel aliandika.

Maafisa wawili wa polisi na mmoja wa washambuliaji waliuawa katika majibizano ya risasi yaliyoanza mwendo wa saa Kumi unusu asubuhi kwenye nyumba iliyoko Tshatshi Boulevard, kulingana na Muhima.

Kanda za video, zinazoonekana kutoka eneo hilo, zilionyesha lori za kijeshi na watu wenye silaha nzito wakipita katika mitaa isiyo na watu katika kitongoji hicho.

Tshisekedi alichaguliwa tena kuwa rais mwezi Disemba katika kura iliyokumbwa na machafuko huku kukiwa na wito wa kura ya maoni kutoka kwa upinzani kutokana na kile walichokisema kuwa ni ukosefu wa uwazi, kufuatia mielekeo ya siku za nyuma ya chaguzi zinazozozaniwa katika nchi hiyo ya Afrika ya kati.

TRT Afrika na mashirika ya habari