Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti ametangaza kuwa nchi hiyo iko tayari kuunganisha nguvu na wawekezaji wa kimataifa ili kupanua sekta yake kibinafsi na kuleta mseto wa uchumi.
Lakini amesema anataka uwekezaji wa haki wenye manufaa kwa pande zote mbili.
"Kipaumbele chetu kabisa kimekuwa kuhakikisha ustawi wa kiuchumi, maendeleo na ustawi wa raia wetu huku tukihifadhi mamlaka yetu, uhuru na usalama," alisema Rais Guelleh, akizungumza katika kongamano la kwanza la uwekezaji wa kimataifa ambapo aliwakaribisha viongozi wa kisiasa na kibiashara zaidi ya 300 kutoka kote duniani.
Rais Guelleh ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kujitosa katika sekta mbalimbali za uchumi wa nchi hiyo, akiwahakikishia fursa nyingi ambazo hazijatumiwa, mazingira rafiki kwa biashara, na usaidizi wa kujitolea wa serikali yake.
Nafasi ya uwekezaji Djibouti
Djibouti ipo katika sehemu nyeti ya uwekezaji , ipo kwenye lango wa bahari wa Bab el-Mandeb mwisho wa kusini mwa Bahari ya Shamu. Hii inamaanisha kuwa iko kwenye njia kuu za meli kati ya Asia na Ulaya, na karibu theluthi moja ya biashara ya baharini duniani ikipita kando ya fuo za Djibouti.
Wataalam wa uchumi wanasema hii inatoa fursa ya kipekee kwa wawekezaji kuwekeza kwa pamoja na serikali katika sekta ya bandari na usafirishaji nchini.
Ili kuwasaidia wawekezaji, nchi hiyo iliunda hazina ya utajiri huru, yaani Soverign Fund, mwaka 2020, ili kuwekeza pamoja na kuchukua hisa katika miradi fulani.
"Ni muhimu kuharakisha uboreshaji wetu. Ni kwa msingi huu ambapo mfuko wa utajiri wa uhuru wa Djibouti uliundwa. Mfuko huo unafungua njia ya kuibuka kwa Djibouti kama kitovu cha ubora,” alisema Rais Guelleh.
Dira ya mwaka 2035 ya nchi hii imejikita katika mseto wa kiuchumi ikiwa ni pamoja na katika sekta kama vile ICT, fedha na viwanda.
Kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika, uchumi wa Djibouti unatarajiwa kukua kwa 6.5% mwaka huu. Nchi inalenga kujitosheleza kwa nishati kwa kutumia 100% aina ya nishati mbadala.
Nchi hiyo tayari inawezesha uwekezaji katika nishati ya upepo na jua, na jotoardhi na kubadilisha taka kuwa nishati na njia nyengine ambazo zinazingatiwa kwa umakini.
Ikiwa na nyaya kumi za chini ya bahari, na tatu zaidi zikiwa zinatarajiwa katika kipindi cha miezi 24 ijayo, Djibouti pia inasema iko tayari kuwa kitovu cha vituo vya data na shughuli zinazohusiana na teknolojia.
Kituo cha Taarifa cha Djibouti ndicho kituo cha kwanza na cha pekee cha kituo cha taarifa kisichoegemea upande wowote katika Afrika Mashariki, chenye ufikiaji wa mifumo yote mikuu ya kimataifa, inayounganisha Ulaya, Mashariki ya Kati na kanda za Asia Pacific na Afrika.
Uboreshaji wa nyaya za mkongo wa intaneti ni kipaumbele cha kikanda na huenda ikatoa suluhu kwa changamoto kama ya sasa ambapo mtandao umekatika tangu 12 Mei 2024, katika Afrika Mashariki na Magharibi kwa sababu ya uharibifu wa nyaya za chini ya bahari.