Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh "anaendelea vizuri sana" kiafya, Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Ilyas Moussa Dawaleh amesema.
Siku ya Jumamosi, kulikuwa na madai, ambayo vyanzo vyake havikuwa wazi, kwamba Rais Guelleh alikuwa amesafirishwa hadi mji mkuu wa Ufaransa Paris kwa matibabu.
Taarifa hizo zimeongeza kuwa mkuu huyo wa nchi mwenye umri wa miaka 76 yuko katika hali mbaya kutokana na tatizo la moyo.
"Samahani wenye chuki , Rais @IsmailOguelleh anaendelea vizuri, vizuri sana," Waziri wa Fedha Dawaleh alisema katika taarifa yake kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter, Jumapili.
'Chuki na kashfa'
“Mtu anaweza kumchukia kiongozi bila ya kuangukia kwenye chuki na kashfa, hadi kuamuru kifo cha Mwislamu mwingine.
"Ndio, yeye (Rais Guelleh) ana tatizo la goti lake la kulia, kwa hivyo ni nini? Yeye kwanza kabisa ni binadamu kama wewe na mimi. Aibu kwa manabii wa adhabu," Dawaleh alisema.
Guelleh amekuwa rais wa Djibouti tangu 1999.
Alishinda muhula wake wa tano Aprili 2021, akipata zaidi ya 97% ya kura katika uchaguzi ambao ulisusiwa na upinzani.