Mkutano huo hufanyika mara kwa mara kutathmini uhusiano wa Uturuki na Afrika ndani ya miaka mitano ijayo./ Picha: AA  

Djibouti itakuwa mwenyeji mkutano wa tatu wa mawaziri unaolenga kutathmini ushirikiano wa Afrika na Uturuki.

Mkutano huo, ambao utafanyika kati ya Novemba 2 na 3, 2024, utaendeshwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan, ambayo ni ishara ya azma ya Uturuki kuwa moja ya washirika wa kimkakati wa Umoja wa Afrika, kuanzia mwaka 2008.

Mkutano huo hufanyika mara kwa mara kutathmini uhusiano wa Uturuki na Afrika ndani ya miaka mitano ijayo.

Kwa mara ya mwisho, mkutano huo ulifanyika jijini Istanbul mwaka 2021, kati ya Disemba 16 na 18. Mkutano mwingine kama huo utafanyika utafanyika katika nchi ya Kiafrika mwaka 2026.

Ziara ya kwanza Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki nchini Djibouti

Mikutano hiyo hufanyika kutathmini maamuzi ya vikao vilivyotangulia.

Istanbul ilikuwa mwenyeji wa mikutano miwili ya kwanza ya tathmini iliyofanyika mwaka 2011 na 2018.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Fidan atakuwa na mazungumzo na mawaziri wenzake kutoka Djibouti na nchi nyingine za Kiafrika, kama sehemu ya Mkutano huo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki kuitembelea Djibouti.

Kipaumbele

Wakati wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje Fidan anategemewa kuweka msisitizo kwenye umuhimu wa Afrika kama sehemu ya kipaumbele cha sera za nje za Uturuki, na kuonesha utayari wa Uturuki kukuza uhusiano.

Waziri Fidan pia atasisitizia namna Uturuki inavyozingatia maendeleo ya kiuchumi, kibinadamu na ya kijamii barani Afrika, kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi za Kiafrika.

Vilevile, Uturuki imezihakikishia nchi za Afrika, utayari wake wa kuunga mkono jitihada za amani na utulivu barani Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje Fidan pia ataunga mkono jitihada za kupaza sauti za Afrika ulimwenguni haswa kwenye siasa za kidunia hasa kwenye majukwaa ya kimataifa, hususani Umoja wa Mataifa, pamoja na Umoja wa Afrika na uanachama wa kudumu wa nchi za G20.

Kukuza mahusiano

Hali kadhalika, Fidan imetoa uhakika wa kukuza na kuimarisha uhusiano wa Umoja wa Afrika na mashirika ya kikanda barani Afrika.

Uturuki pia itathibitisha dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na washirika wa Afrika katika kutekeleza miradi ndani ya Mpango wa Utekelezaji wa Pamoja wa 2022-2026.

Mkutano huo pia utahusisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi 14 za Kiafrika.

Nchi hizi ni pamoja na Djibouti, Mauritania, Angola, Jamhuri ya Congo, Ghana, Comoro, Sudan Kusini, Chad, Equatorial Guinea, Libya, Nigeria, Zimbabwe, Zambia, na Misri.

Ushirikiano

Wawakilishi wa Tume ya Umoja wa Afrika wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

Wakati wa mkutano wa mwaka 2021, Mpango wa Utekelezaji wa Pamoja wa mwaka 2022-2026 uliidhinishwa, huku ukianisha miradi tofauti ya ushirikiano.

Maeneo hayo ni pamoja na nyanja ya Ulinzi na Usalama, Utawala, Uwekezaji, Biashara, Viwanda, Vijana, Maendeleo ya Wanawake, Maendeleo ya Miundombinu, Kilimo na maendeleo ya mifumo ya afya.

Juhudi zinaendelea kutekeleza maamuzi na miradi ya pamoja iliyoanzishwa katika mkutano huo.

Maeneo ya kuangazia

Mkutano ujao wa Mapitio ya Mawaziri mnamo Novemba 2 hadi 3, 2024, utajikita katika kukagua maendeleo ya maamuzi yaliyofanywa kwenye Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Uturuki na Afrika huko Istanbul mnamo 2021; kutathmini maendeleo kuelekea malengo yaliyowekwa katika "Mpango wa Utekelezaji wa Pamoja wa 2022-2026"; na kuchunguza hatua zinazowezekana za kuimarisha zaidi ushirikiano wa Uturuki na Afrika.

Inatarajiwa kwamba, mwishoni mwa mkutano huo hati mbili - "Tamko la Pamoja" na "Ripoti ya Pamoja ya Utekelezaji wa 2022-2024" - zitapitishwa. Hati hizi zinatayarishwa kwa pamoja na Uturuki na Tume ya Umoja wa Afrika.

Azimio la Pamoja litathibitisha dhamira ya pamoja ya kuimarisha uhusiano wa Uturuki na Afrika katika nyanja mbalimbali na kushughulikia maendeleo ya kikanda, bara na kimataifa yanayoathiri Uturuki na nchi za Afrika.

Ripoti ya Pamoja ya Utekelezaji itatoa muhtasari wa shughuli za Uturuki baina ya nchi mbili na kimataifa barani Afrika kuelekea malengo ya Mpango wa Utekelezaji wa Pamoja wa 2022-2026 kutoka 2022 hadi 2024, na pia kutoa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano wa sasa.

TRT Afrika