Maafisa wa upelelezi wa mauaji wameendelea na uchunguzi kuhusu mauaji ya kutatanisha ya watu ambao miili yao ilipatikana siku ya Ijumaa kwenye machimbo yaliyotelekezwa eneo la Villa, Mukuru kwa Njenga.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mohamed Amin, idadi ya maiti zilizotolewa kwenye machimbo hayo ni sita, zote za kike, huku miili hiyo ikianza kuoza.
Miili hiyo, ambayo ilihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti, ikisubiri kufanyiwa upasuaji, ilikuwa imefungwa kwa karatasi za nailoni.
"Ugunduzi huo mbaya ulipatikana katika machimbo yaliyotelekezwa, ambayo kwa sasa yamejaa maji na kutumika kama eneo la kutupa taka. Wafanyakazi wa Uchunguzi wa Eneo la Uhalifu (CSI) kutoka Embakasi walifika haraka katika eneo la tukio, na kuchukua rekodi ya eneo hilo,” DCI ilisema.
Kulingana na DCI, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu wote wameuawa kwa njia moja.
“Wapelelezi wa mauaji na maafisa kutoka Idara ya Uchunguzi ya DCI kwa sasa wanachanganua sampuli ili kubaini miili hiyo. Eneo hilo limefungwa na kuwa eneo la uhalifu huku uchunguzi ukiendelea,” DCI iliongeza.
"Tunaposubiri matokeo ya uchunguzi wa vifo na uchunguzi wa kitaalamu wa kimaabara, DCI inawaomba wananchi kushirikiana na mamlaka huku uchunguzi ukiendelea."
Hapo awali rais wa chama cha mawakili nchini Kenya Faith Odhiambo kupitia mtandao wa X, ametoa wito wa kuchunguzwa kwa madai ya kupatikana miili hiyo karibu na Kituo cha Polisi cha Kware.