Ikiwa imebaki miezi mitatu tu kabla ya kufanyika kwa mkutano kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi COP27 nchini Misri, mataifa ya Afrika yamepaza sauti kwa viongozi wa dunia yakitaka rasilimali fedha na uwezeshaji wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mpango wa Kisera kwa Tabianchi CPI, Afrika inazalisha asilimia 4% ya gesi ya carbon dioxide hewani licha ya kuwa na humusi(1/5) tu ya jumla ya idadi ya watu duniani, lakini bara hilo limeathrikia zaidi na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
“Jukumu hili lisilo la usawa limetwikwa Bara la Afrika ambalo linachangia 4% tu ya uzalishaji wa gesi hewani lakini madhara ya mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni makali zaidi kwa upande wa Afrika na watu wake. Hili linaweza tu likatafsiriwa kama udhalimu mkubwa,” alisema Waziri wa masuala ya kigeni wa Misri Sameh Choukry kwenye mkutano wa kujiandaa kwa ajili ya COP27 Libreville, nchini Gabon.
Afrika haijawahi kusita kuomba makongamano ya kujadili mabadiliko ya tabianchi ikiwa na lengo la kupata rasilimali fedha za kuwezesha kupigana na mabadiliko hayo. Hatahivyo uwezeshaji Afrika ilifanikiwa kuupata mwaka 2020 ni dola za kimarekani bilioni 29 licha ya kusadikiwa kuwa Bara hilo lilihitaji takriban dola za kimarekani bilioni 250 ili kupigana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mfano nchi kama Jamhuru ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) ambayo ilitarajia kupata dola bilioni 10 kwenye mkutano wa COP26 ilifanikiwa kupata dola milioni 500.
Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB), mabadiliko ya tabianchi yameathiri pakubwa Pato la Mataifa ya Afrika GDP. “Bara la Afrika limeshuhudia Pato lake likipungua kwa kati ya asilimia 5% hadi asilimia 15% kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kati yam waka 2016 na 2019, mataifa ya Afrika kwa ujumla yalipokea dola za kimarekani bilioni 18.3 kama bajeti ya tabianchi. Bajeti hio inakadiriwa kufikia dola bilioni 127.2 itimiapo kati ya 2020 mpaka 2030.” Ripoti ya AfDB ilionesha.
Athari hatari
Madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika bara la Afrika yataendelea kusababisha joto jingi kupita kiasi, ukame na mafuriko. Ongezeko la joto duniani kwa upande wa Afrika litafikia nyuzi +1.5%. Makadirio yamefanyika hilo likitokea.
Kwa hali hiyo basi shughuli za ukulima – kwa mfano wa kilimo cha mzeituni katika Afrika ya Kaskazini na kahawa katika Afrika ya Mashariki kitaathirika pakubwa.
Ongezeko la magonjwa yanasababishwa na ‘vector’ litashuhudiwa kama vile; ugonjwa wa malaria katika Afrika ya Magharibi na Kati pamoja na homa ya dengue katika Kusini na Mashariki ya Afrika.
Kwenye suala uvuvi pia kuna hofu kuwa utapungua kwa asilimia 50% katika Afrika ya Magharibi.
Kwa nyuzi joto +2% katika Afrika ya Kaskazini, basi asilimia 20% ya wanyama wapo katika hatari ya kufa huku mazao ya chakula katika Afrika ya Magharibi yakitarajiwa kupungua kwa asilimia 42%. Aidha asilimia 90% ya miamba ya matumbawe nchini Madagascar ikitarajiwa kuharibika huku milima ya Ruwenzori na Kilimanjaro ikiwa katika hatari ya kutoweka.
Nafasi kubwa iliyoko
Licha ya kuwa Bara la Afrika linaonekana kuwa katika hali mbaya ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, Afrika inayo nafasi na uwezo mkubwa wa kujisitiri kutokana na madhara haya. Aidha wapo wanaosadiki kuwa Afrika inaweza hata ikawa suluhisho la mabadiliko ya tabianchi kwa dunia.
Afrika inayo nafasi kubwa ya kuangalia na kuwekeza kwenye Kilimo endelevu hususan cha Kilimo Mseto yaani ‘agroforestry’ kinachohusisha kilimo cha mimea na chakula sambamba na upandaji miti. Mbinu huchochea rutuba ya udongo na inatumika sana nchini Cameroon kurejesha misitu iliyoharibiwa.
Katika mwaka wa 2007, Muungano wa Afrika(AU) ulizindua mradi wa ‘Great Green Wall’ ambao lengo lake ni upandaji wa mamilioni ya miti kama hatua moja ya kurejesha misitu na kupunguza ueneaji wa jangwa, huku madhumuni makubwa yakiwa ni kuinua hali ya maisha ya binadamu na kupigana na uhaba wa chakula.
Bara la Afrika pia linaweza likatumia vizuri ongezeko la idadi ya watu wake na ukuaji wa miji kuunda makazi ya watu yanayokumbatia teknolojia ya kijani inayohakikisha kuwa hatarakati za binadamu ni zilizo rafiki wa mazingira.
Gabon, Bingwa wa dunia wa kuhifadhi mazingira
Kuanzia Jumatatu, taifa la Gabon katika mji wa ke mkuu wa Libreville litakuwa mwenyeji wa Mkutano wa ‘Africa Climate Week’ ambao ni mpango mzima wa Umoja wa Mataifa kujadili mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kutatua madhara yatokanayo na mabadiliko hayo. Zaidi ya watu 1000 watahudhuria wakiwemo viongozi wa kisiasa, waakilishi wa mashirika ya kimataifa pamoja na viongozi wa asasi za kiraia, kujadili maazimio ya mkutano wa COP26.
“Lengo hapa ni kuzungumza kwa sauti moja kama watu wa Afrika kuelekea mkutano wa COP27 na kubuni mapendekezo yaliyo na mashiko.” Alisema Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba.
“Wakati umewadi sasa kama Afrika kuchukua mustakabali na hatima yetu mkononi,” aliongeza Rais Ali Bongo huku akikosoa Jumuiya ya Kimataifa kwa kufeli katika utekelezaji wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi ulioafikiwa katika Mkutano wa COP21 Jijini Paris ambapo mataifa yalikubali kupunguza gesi joto ili kufikia lengo la dunia la kutokuongezeka kwa wastani wa joto la dunia kwa zaidi ya nyuzi 20C au 1.50C
Mkutano huu wa ‘Climate Week’ kufanyika nchini Gabon sio kwa bahati mbaya. Taifa la Gabon limesifiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwa mstari mbele kupigana kutunza mazingira na kupigana na ongezeko la joto duniani. Gabon ni taifa lenye idadi ya watu wasiozidi milioni 10 na lipo katikati ya msitu wa kitropiki wa Afrika ya Kati ujulikanao kama “pafu la pili la dunia” baada ya Amazon.
Gabon ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kutunukiwa kwa rasilimali fedha za kimataifa kutokana na mchango wake wa ufyonzaji wa gesi ya C02 kupitia programu za kutunza misitu, ambayo inafunika zaidi ya 90% ya eneo lake.