Bunge la Uganda limeamua kuwasimamisha wabunge waliohuska katika mzozo ndani ya bunge Jumatano asubuhi.
Limetoa orodha ya wabunge 12 ambao wameadhibiwa kufuatia purukushani hizo bungeni.
Spika amewaamuru wabunge hao wasihudhurie vikao na waondoke katika ukumbi wa bunge.
“Ninaendelea kuwataja wabunge na kuwasimamisha kuhudhuria vikao vitatu mfululizo vya Bunge hili. Wajumbe hao wamesimamishwa kazi mara moja kutoka Bungeni kwa muda huo," spika wa bunge Anita Among alisema.
Spika alisimamisha bunge kwa dakika 15 ili kuyatimiza haya.
"Pia nasisitiza Kanuni ya 88(2) kuamuru Wabunge waliotajwa hapo juu wajitoke mara moja kwenye Bunge na kwa mujibu wa agizo la Askari wa bungeni waondoke nje ya Ukumbi ," amonga alisema.
Machafuko yalizuka bungeni wakati wa kikao cha kujadili Muswada wa Kitaifa wa Marekebisho ya Kahawa wa 2024 uliokumbwa na utata.
Imeripotiwa kuwa mbunge wa Kilak Kaskazini Anthony Akol alianza kuzozana na Mbunge wa Manispaa ya Mityana Francis Zaake wakati wa kikao hicho na video inaoinyesha walitupiana mangumi.
Wawili hao ni kati ya waliosimamishwa kwa muda.
Spika wa bunge ameomba radhi kwa kitendo alichoita cha kinyama kwa mbunge Francis Zaake baada ya kupigwa na mbunge mwenzake Anthony Akol kufuatia mabishano makali kuhusu jinsi ya kuketi katika bunge.
"Nataka kuandikisha msamaha wangu kwa kile kilichotokea kwa mwenzetu kwa dhati, ambayo haikufaa. Kilichomtokea Zaake hakikufaa. Kufuatia yale yaliyomkuta Zaake asubuhi ya leo Bungeni, nitarejelea Kanuni ya 89 inayosema kwamba iwapo spika ataona kuwa mwenendo wa mjumbe hauwezi kushughulikiwa ipasavyo, anaweza kuwataja wajumbe hao wazi,” alisema.